
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza na Menejimenti ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi hiyo, tarehe 24 Novemba, 2025 jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi hiyo tarehe 24. Novemba, 2025 jijini Dodoma. kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray na Kushoto kwake ni Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bwana Mick Kiliba.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akitoa neno kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kuzungumza na Watumishi wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakati wa ziara ya kikazi ya viongozi hao katika Ofisi hiyo tarehe 24. Novemba,2025 jijini Dodoma.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bwana Mick Kiliba akitambulisha Menejimenti ya Ofisi yake wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tarehe 24. Novemba, 2025 jijini Dodoma

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavery Daudi akifurahia jambo alipokuwa akimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi hiyo, tarehe 24 Novemba, 2025 jijini Dodoma.

Katibu mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma,Bw. Juma Mkomi akitaka ufafanuzi juu ya utendaji kazi wa kituo cha huduma kwa Mteja wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Ofisi hiyo Mhe. Ridhiwani Kikwete, tarehe 24. Novemba, 2025 jijini Dodoma
Na Antonia Mbwambo-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Menejimenti ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuharakisha na kuweka wazi mchakato wa ajira 12,000 zilizotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 14 Novemba, 2025 jijini Dodoma.
Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 24.11.2025 ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika taasisi hiyo tangu alipoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 18 Novemba, 2025 kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Amesema moja ya ahadi za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Utumishi wa Umma unakuwa bora katika kutekeleza majukumu ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi na kuongeza kuwa ili kuhakikisha hili linaanza kutekelezwa aliahidi kutoa vibali vya ajira 12,000 kwa Kada ya Elimu watumishi 7,000 na Kada ya Afya, watumishi 5,000.
“Kibali cha ajira kimeshatolewa, nawashukuru kwa kuanza kufanyia kazi, ni jambo zuri, ni mategemeo yangu kuwa majawabu ya maelekezo ya Mhe. Rais tutayaona hivi karibuni, hakikisheni mnasimamia kwa ukamilifu, mchakato wote wa ajira hizi uwekwe wazi ili kuondoa dhana potofu ya kuwa kuna upendeleo katika kutoa ajira.” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Ameitaka Menejimenti hiyo kuongeza kasi ya kuratibu mchakato wa ajira “Tuangalie changamoto zinazokwamisha uharakishaji wa mchakato wa ajira ili tuweze kutatua na kuendelea na kukamilisha kwa wakati.” Ameongeza.
Pia, ameielekeza Menejimenti hiyo kuzingatia maadili katika kusimamia mchakato huo wa ajira ili kuhakikisha wanapatikana watumishi sahihi na wenye vigezo. kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, ameisisitiza Menejimenti hiyo kutoonea watumishi walio chini yao bali wawaelekeze kwa upendo. “Tusimamie maadili katika utekelezaji wa majukumu yetu, tusionee watumishi walio chini yetu, tuzingatie taratibu za utendaji kazi.” Ameongeza
Pamoja na maelekezo aliyoyatoa kwa Menejimenti hiyo, Mhe. Kikwete ameomba ushirikiano katika utekelekezaji wa majukumu ya Serikali ili kufikia malengo ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa ustawi wa taifa
Amewapongeza kwa kutekeleza maelekezo ya Wabunge katika kuendesha usaili ngazi ya mkoa na wanaopangiwa kazi kupokelea barua za ajira katika mikoa yao.
“Nawashukuru, pamoja na kuwa nilikuwa katika Ofisi nyingine lakini mmefanya kazi nzuri, tuendelee tusirudi nyuma, suala la kufanya mahojiano mikoani na kuchukua barua za ajira mikoani limeweza kupunguza kadhia.” Amesema.
Katika hatua nyingine, amewapongeza kwa kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja (call centre) kwani itapunguza adha kwa wenye uhitaji wa huduma na kuwasisitiza kuwaweka watumishi wenye kauli nzuri.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray amesisitiza ushirikiano toka kwa Menejimenti hiyo. “Tumekuja kujitambulisha, ninaomba ushirikiano wenu, tufanye kazi kwa pamoja, tutatue kero za wananchi kama ambayo Rais wetu anatamani iwe.
Aidha amepongeza kazi inayofanyika katika taasisi hiyo. “Ni mara yangu ya kwanza kufika katika jengo hili, ni masaa machache nimetembelea katika jengo hili lakini napenda niwapongeze nimeona kazi zinavyofanyika, hongereni sana.
Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Bwana Mick Kiliba akielezea majukumu ya Taasisi hiyo, amemshukuru Mhe. Waziri na Viongozi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora aliombatana nao kwa kuona umuhimu wa kutembelea katika Ofisi hiyo na kuwahimiza uwajibikaji kwa maslahi mapana ya taifa.
Akiainisha mafanikio mbalimbali ya Taasisi hiyo, Bw. Kiliba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kumiliki jengo lao ambapo sasa watumishi wote wako katika jengo moja na kuwaongezea bajeti ya utekelezaji wa majukumu yao ya masuala ya ajira.

Post A Comment: