Na Mwandishi wetu -Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imeendelea kuiishi kauli mbiu ya "Kazi na Utu" kwa kufanya ziara maalum ya kuwatembelea wanafunzi wenye mahitaji maalum waliopo vyuo vikuu Nchini kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwasaidia wanafunzi hao kutimiza malengo yao.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga kwenye ziara yake alipotembelea wanafunzi wenye ulemavu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mhe. Nderiananga amesema kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wanafunzi wenye ulemavu kutatua changamoto zinazowakabili ili kuhakikisha wanafikia malengo yao ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi itakayowezesha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2025-2050.
Aidha, Nderiananga ametoa wito kwa vijana wenye ulemavu kuwaelimisha watu wengine juu ya dhima ya kutunza amani, kwa sababu amani ikikosekana watu wenye ulemavu wanaathirika zaidi kutoka na kukosa uwezo wa kujiokoa.
Awali, Mkurugenzi wa Elimu Maalum Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Magreth Matonya aliwaambia wanafunzi wenye ulemavu kuwa kupata mkopo asilimia 100 ni haki yao hivyo watashirikiana na Bodi ya Mikopo (HESLB) ili kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu ambao hawajapata mikopo wanapata kwa wakati.
"Serikali imekuwa ikitoa fedha kila mwaka kwa ajili ya kununulia vifaa vya wanafunzi wenye mahitaji maalum, uhitaji bado upo lakini si mkubwa kama ilivyokuwa hapo awali kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali. Ameongeza Dkt. Matonya
Kwa upande wake Bi. Grace Daniel mwanafunzi mwenye ulemavu wa Ngozi katika Chuo Kikuu cha DODOMA ameiomba Serikali na Sekta binafsi kuendelea kutoa kipaumbele cha ajira kwa watu wenye ulemavu wenye sifa.
Naye Bw. Jackson James mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa vifaa kama vile Viti mwendo vinavyowawezesha kuhudhuria vipindi kwa urahisi huku akiiomba Seriklai kuwafiki wanafunzi wenyeulemavu Vijijini.
= MWISHO=

Post A Comment: