Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati, Bi. Neema Mbuja amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo ili kufikia malengo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80% ya wananchi wanatumia nishati safi katika shughuli za upishi.
Akizungumza leo Novemba 25, 2024 katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC1, katika kipengele cha Jikoni na Chigo, Bi. Mbuja amesema kuwa mahojiano hayo ni sehemu ya muendelezo wa ziara ya Wizara ya Nishati katika vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida na umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.
Aidha, amesisitiza kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na jamii katika kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya nishati safi inawafikia wananchi wengi zaidi, hivyo kuchochea utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuimarisha afya, mazingira na ustawi wa jamii kupitia matumizi ya nishati rafiki.



Post A Comment: