Serikali kupitia Mamlaka ya Udhbiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewajengea uwezo maafisa maendeleo ya jamii ili waendelee kuwa daraja muhimu la kuwasaidia vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kuzipata fursa za zabuni zilizotengwa kwaajili yao.


Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo yaliyotolewa na PPRA kwa maafisa maendeleo ya jamii na maafisa ununuzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Eliya Luvanda, amesema ni jukumu la watendaji hao kuwajengea uwezo wanufaika ili waweze kuingia kwenye ushindani wa zabuni zinazotolewa na serikali.

Luvanda amesema kuwa vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu wanapaswa kujengewa uwezo ili kunufaika na asilimia 30 ya bajeti ya tenda za Serikali, ambayo mwaka huu wametengewa bajeti ya zaidi ya Shilingi Trilioni Tano.

Aidha, amewata maafisa hao kutumia vyema elimu waliyopewa na PPRA, kuhakikisha wanatoa elimu zaidi kuwaandaa na kuwawezesha wahusika ili yaweze kuitumia fursa hiyo muhimu inayotolewa na serikali yenye lengo la kuwainua kiuchumi.

Afisa Tehama Mwandamizi wa PPRA, Bw. Damasi Makweba, amesema mafunzo hayo yamebuniwa ili kuongeza uelewa wa watendaji wanaohusika moja kwa moja na mchakato wa kuibua na kusajili makundi maalum katika maeneo yao.

Amesema zaidi ya washiriki 115 kutoka kata mbalimbali mkoani Iringa, wanatarajiwa kutekeleza kwa vitendo mafunzo hayo kwa kuhakikisha vikundi vyote vilivyopo vinatambuliwa na kusajiliwa ili viweze kunufaika na fursa hiyo kupitia Mfumo wa NeST.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Iringa, Bi. Mwatumu Dosi, amesema halmashauri hiyo imeshasajili vikundi sita, na kimoja tayari kimenufaika na mpango huo wa serikali, na kuongeza kuwa uhamasishaji na utoaji wa elimu utaendelea kufanyika ili vikundi vingine vingi zaidi viweze kuingia kwenye mfumo huo.




Share To:

Post A Comment: