Articles by "NJOMBE"
Showing posts with label NJOMBE. Show all posts

 


Kuanzishwa kwa Kampasi ya Njombe ya Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia Mradi wa HEET kumeanza kutaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, ajira na uchumi wa mkoa wa Njombe. Mradi huu unalenga kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Kusini na kuchochea maendeleo ya miundombinu ya kisasa.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, alipokutana na viongozi wa Mkoa wa Njombe akiwemo Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala na Kamati ya Ulinzi na Usalama. Alisema Njombe imepata fursa ya kipekee kwa kuwa na matawi ya vyuo vikuu zaidi ya kimoja.

Prof. Nombo alieleza kuwa uwepo wa kampasi hiyo utachochea shughuli za kiuchumi katika maeneo jirani. Alisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba za makazi, hosteli za wanafunzi, na vituo vya huduma kama maduka na migahawa  ili kuandaa mazingira rafiki kwa wanafunzi na watumishi wa kampasi hiyo.

Aliongeza kuwa ongezeko la wanafunzi litahitaji huduma bora za afya, usafi wa mazingira, Miundombinu ya  TEHAMA. Alitoa wito kwa taasisi husika kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati katika eneo la Mradi kabla ya kuanza Kwa udahili wa Wanafunzi hasa kwa kuzingatia mfumo wa “blended learning” unaotegemea miundombinu ya intaneti ya uhakika.

Prof. Nombo aliipongeza Njombe kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya elimu. Aliahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na mkoa huo kuhakikisha mradi wa Kampasi ya Njombe unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

 


Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb), amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Makambako na Wanging’ombe.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, alimkaribisha rasmi na kumshukuru kwa uamuzi wa kufika binafsi kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi. Alisisitiza kuwa ofisi ya mkoa iko tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliopangwa.

Miradi hiyo inatekelezwa chini ya Mradi wa Miji 28, ambao unalenga kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa miji nchini. Kwa upande wa Njombe, zaidi ya shilingi bilioni 80 tayari zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi hiyo, kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.

Akizungumza na viongozi na wataalamu wa maji, Mhe. Aweso alisisitiza kuwa fedha zipo, hivyo hakuna sababu ya ucheleweshaji. Aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora wa hali ya juu kabla ya Desemba 2025, muda uliopangwa kwa maeneo ya Njombe na Makambako.

“Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mkandarasi atakayeshindwa kutimiza wajibu wake,” alisisitiza Waziri Aweso.

Ziara hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na kuendeleza jitihada za kumtua mama ndoo kichwani.



















 


Serikali ya Tanzania inaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu  katika bandari ya Dar es Salaam ili kupunguza changamoto kubwa ya usafirishaji wa bidhaa ikiwemo matunda ya Parachichi kwa kupeleka bandari zilizopo nchi jirani.

Afisa mtendaji mkuu wa Tanzania Horticulture Association (TAHA) Dkt.Jacqueline Mkindi ameeleza hayo mkoani Njombe mara baada ya wawekezaji kueleza changamoto  hiyo ulipokuwa ukifanyika uzinduzi wa vituo vya kukusanyia mazao ya Horticulture mkoani humo.

"Kwa sasa hivi 80% ya kontena za Pachichi kwa hawa wasafirishaji bado zinapita Mombasa na unaona wawekezaji wako tayari kupita Mombasa na sio Dar kwanini ni kwasababu ya uwezo kuondokana na mambo mengine mengi lakini tunashukuru serikali kunamaendeleo makubwa yanafanyika Dar"

Amesema changamoto hizo zinakwenda kutatuliwa kwa kipindi kifupi kijacho kwasababu awali asilimia 100% wawekezaji walikuwa wakipita Mombasa na mabadiriko makubwa yameanza ambapo kuanzia mwaka 2021 asilimia 15% mpaka 20% ya kontena zinapita bandari ya Dar es Salaam.

Awali Meneja wa Avodemia, Mohamed Adam Jee ambao ni wawekezaji na wasafirishaji wa Parachichi,amesema kuwa uhitaji wa Parachichi za Tanzania huko Duniani ni mkubwa lakini wamekuwa wakipata shida na kutumia gharama kubwa kusafirisha zao hilo huku wakilazimika kutumia bandari ya Nje ya Tanzania kutokana na changamoto ya miundombinu iliyopo katika bandari ya Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Dkt.Hussein Mohamed Omari amesema Serikali inafanyia kazi changamoto hizo ambapo pia Imeongeza bajeti Kwenye sekta ya kilimo kutoka Bilioni 294 hadi Trioni 1.28 na kwamba ujenzi wa vituo vya kupimia na kukusanyia Parachichi vilivyo jengwa na TAHA ni mkombozi kwa wakulima.

Jumla ya vituo vitano vya kukusanyia mazao ya horticulture vimezinduliwa mkoani Njombe ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu ili kupunguza upungufu wa upotevu wa mazao.






Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Balozi Dkt.Pindi Chana (Mb) ameshiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Shule ya Msingi Idofi kwenye Kijiji cha Idofi, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Mkoani Njombe leo Mei 3,2025.

Akizungumza katika mapokezi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amesema Mwenge huo utakimbizwa  jumla ya kilomita 869.7 kwa muda wa siku sita katika Wilaya nne za Mkoa wa Njombe ambapo utazindua, kukagua, kufungua, kugawa na kutembelea jumla ya miradi 62 yenye thamani ya shilingi bilioni 17.6 Mkoani humo.

Mwenge huo uliongozwa na Kiongozi wa  mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Bw. Ismail Ali Ussi kutoka Unguja Kaskazini.










Kamati ya Siasa ya halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Njombe imetoa maelekezo kwa kamati za siasa wilaya zote mkoani humo kuwachukulia hatua wanachama na viongozi wote wa chama hicho wanaoandika maneno yenye kukejeli na kutukana viongizi mitandaoni.

Akitoa taarifa ya kikao cha kawaida cha kamati ya Siasa kilichofanyika mkoani humo,katibu wa Siasa na Uenezi mkoa wa Njombe Josaya Luoga amesema kikao hicho kilichokuwa na lengo la kujadili mambo mbalimbali ya Chama lakini pia kimetoa maelekezo hayo ili kudhibiti sintofahamu zinazotengenezwa na kuharibu kazi za Chama.

"Kamati ya Siasa ya halmashauri kuu ya mkoa imetoa maelekezo kwa kamati za Siasa  za wilaya na kamati za maadili kuhakikisha zinafanya kazi ya kuwaita watu wote wanaochapisha mitandaoni maneno yanayo ashiria kutengeneza sintofahamu kwenye makundi sogozi na kuwachukulia hatua"amesema Luoga

Amesema "Wale wote ambao wataonekana kweli wameandika na kuthibitika watachukuliwa hatua kali kuhakikisha chama kinakuwa tulivu kuelekea uchaguzi 2025 tuwapate viongozi ambao watakwenda kufanya kazi za wananchi kwa utulivu"

Luoga amewataka wanachama na viongozi wa Chama hicho kuchukua tahadhari na mandishi yanayochapishwa mitandaoni ambapo ametoa rai kwa wanachama kuandika maneno yanayolenga umoja na mshikamano wa Chama cha Mapinduzi.

Wakati Kanisa Katoriki likiadhimisha Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo na siku ya wafanyakazi Duniani,Hosptali ya St Joseph Ikelu iliyopo kata ya Utengule halmashauri ya mji wa Makambako inatoa huduma ya vipimo bure kwa wananchi wenye nia ya kujua afya zao ili waweze kuanza matibabu.

Akizungumza wakati zoezi la vipimo likiendelea Daktari wa hospitali hiyo,Dkt.Polikap Nyengela amesema vipimo vinavyotolewa ni pamoja na kipimo cha Kisukari,Macho,Tezi dume,Saratani ya Matiti,shinikizo la damu na hali ya lishe,ambapo lengo la kutoa huduma hiyo bure ni kurejesha kwa jamii kile walichokipata ili kuwasaidia wananchi kutambua hali.

Amesema kwa sasa watu wengi wanakumbwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu hali ambayo inapekekea kuathirika kwa mfumo wa mwili na kusababisha wengi wao kuishi na magonjwa kwa muda mrefu bila kujua kama wanaumwa kutokana na kutokuwa na kawaida ya kupima afya zao.

"Tunarudisha kwa jamii kile ambacho tumefanikiwa kukipata na zoezi hili tunalifanya kwa muda wa siku mbili tarehe moja leo (jana) na leo tarehe mbili"amesema Nyengela

Dkt.Nyengela amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa bila kupata vipimo sahihi vya wataalamu wa afya kwa kuwa inasababisha wengi wao kuathirika kutokana na kutumia dawa zisizo sahihi.

"Watu wengi wanakumbwa na changamoto halafu wanaenda kununua dawa bila vipimo kwa hiyo ni vizuri kuchukua vipimo ili kupata matibabu sahihi"ameongeza Dkt.Nyengela

Baadhi ya wananchi akiwemo Onesmo Ngimbuchi,Lupeta Mlelwa na Eva Mhala ambao wamejitokeza kupata vipimo hivyo wameshukuru uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuja na zoezi la kutoa vipimo bure kwani wengi wao wamekuwa wakishindwa kupima afya zao kutokana na kukosa fedha.

"Wengi tulikuwa tunashindwa kumuda badhi ya vipimo kwa hiyo tulivyoona hii fursa tumeona ndio nafasi ya kuitumia"wamesema wanufaika

Kanisa Katholiki Duniani huadhimisha Jubilei ya Ukristo kila baada ya miaka 25 ikiwa ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi,Upatanisho na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya kitubio.

 


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amewataka waajiri kuhakikisha wanatoa stahiki za wafanyakazi kwa wakati ili kuepusha migogoro isiyo na tija kazini. 

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika wilayani Ludewa, Mhe. Mtaka alisisitiza kuwa waajiri wanapaswa kuwa nguzo ya mafanikio kwa wafanyakazi wao badala ya kuwa chanzo cha migogoro. 

Aliongeza kuwa utoaji wa haki kwa wakati ni msingi wa ufanisi, utulivu na maendeleo katika taasisi na jamii kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Mtaka alitumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi, hususan vijana, kuwekeza katika sekta ya kilimo, biashara na maeneo mengine ya uzalishaji mali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Alisema mkoa wa Njombe una fursa nyingi za maendeleo ambazo zinahitaji ujasiri, ubunifu na ushirikiano baina ya wananchi na serikali ili kuzitumia ipasavyo.

Katika maadhimisho hayo, Mkuu huyo wa Mkoa alipokea tuzo ya pongezi kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kusimamia vyema maendeleo ya kiutawala na huduma za kijamii.

Tukio hilo lilipambwa pia na tangazo lililowagusa moja kwa moja wafanyakazi—ongezeko la mshahara wa kima cha chini kutoka Shilingi 370,000 hadi Shilingi 500,000, kama alivyoeleza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, sekta binafsi pamoja na wafanyakazi kutoka maeneo tofauti ya mkoa wa Njombe. Hafla hiyo iliashiria mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi, sambamba na kutoa shukrani za dhati kwa Rais kwa kusikia kilio cha wafanyakazi na kuchukua hatua ya kihistoria kwa kuongeza mishahara.





Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametoa wito kwa watumishi wa umma kuwa wabunifu katika kutafuta fursa za kiuchumi huku akiwatahadharisha dhidi ya maisha ya "maigizo" na utegemezi wa mikopo kutoka taasisi zenye masharti kandamizi. 

Akizungumza Mei 1, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Mhe. Mtaka aliwataka watumishi kutumia muda wao wa kazi kugundua na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuongeza kipato halali nje ya mishahara yao ya kila mwezi.

“Acheni kuishi kwa ‘show off’. Tujifunze kujiwekea akiba, kuwekeza kwenye kilimo, biashara, na sekta ya misitu. Mnapokuwa kazini mkiona fursa, wekezeni. Msisubiri hadi mstaafu,” alisema Mtaka. 

Akiendelea kuzungumza kwa Msisitizo jambo hilo Mhe. Mtaka  alisema ni umuhimu kufanya maandalizi ya maisha ya baada ya ajira ambapo Mtaka alitaja wimbo wa ...msanii Alichoke uitwao Fainali Uzeeni... kuwa na ujumbe mzito kwa watumishi wa umma kuhusu umuhimu wa kupanga maisha mapema.

“Unapoomba kuongezewa mshahara ni kweli – lakini ukiongezewa, unautumiaje? Kuna watumishi wanakopa ili kufanyia matumizi yasiyo sahihi. Hii haipendezi,” aliongeza kwa kusisitiza.

Aidha, Mhe. Mtaka aliwapongeza watumishi wote waliotunukiwa zawadi za utumishi bora katika maadhimisho hayo, akiwahimiza kuendelea kujituma na kuwa mfano kwa wenzao katika utumishi wa umma.







 


Mkoa wa Njombe umezindua rasmi kampeni ya uhamasishaji wa utoaji wa dozi ya pili ya chanjo ya Polio kwa njia ya sindano kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 16 Aprili, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Mhe. Juma Sweda, aliongoza hafla hiyo na kusisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo muhimu ili kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa Polio.

Katika hotuba yake, Mhe. Sweda alieleza kuwa lengo la nyongeza hii ya chanjo ni kuhakikisha kuwa watoto wote chini ya miaka mitano wanapata kinga kamili dhidi ya virusi vya Polio, vinavyoweza kusababisha ulemavu wa kudumu. Alibainisha kuwa chanjo hiyo ya sindano itatolewa kwa watoto wenye umri wa wiki 14 kwa dozi ya kwanza na dozi ya pili wakifikisha miezi 9.

Aidha, aliwashukuru wataalamu wa afya kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka waendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa chanjo, kuhakikisha ubora na usalama wake, pamoja na kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto katika vituo rasmi vya kutolea huduma hiyo.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa afya, wawakilishi wa taasisi za kijamii, viongozi wa dini, pamoja na wananchi walioalikwa kushiriki kwenye tukio hilo muhimu kwa ustawi wa afya ya mtoto katika Mkoa wa Njombe.