Wakati Kanisa Katoriki likiadhimisha Jubilei ya mwaka 2025 ya Ukristo na siku ya wafanyakazi Duniani,Hosptali ya St Joseph Ikelu iliyopo kata ya Utengule halmashauri ya mji wa Makambako inatoa huduma ya vipimo bure kwa wananchi wenye nia ya kujua afya zao ili waweze kuanza matibabu.

Akizungumza wakati zoezi la vipimo likiendelea Daktari wa hospitali hiyo,Dkt.Polikap Nyengela amesema vipimo vinavyotolewa ni pamoja na kipimo cha Kisukari,Macho,Tezi dume,Saratani ya Matiti,shinikizo la damu na hali ya lishe,ambapo lengo la kutoa huduma hiyo bure ni kurejesha kwa jamii kile walichokipata ili kuwasaidia wananchi kutambua hali.

Amesema kwa sasa watu wengi wanakumbwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu hali ambayo inapekekea kuathirika kwa mfumo wa mwili na kusababisha wengi wao kuishi na magonjwa kwa muda mrefu bila kujua kama wanaumwa kutokana na kutokuwa na kawaida ya kupima afya zao.

"Tunarudisha kwa jamii kile ambacho tumefanikiwa kukipata na zoezi hili tunalifanya kwa muda wa siku mbili tarehe moja leo (jana) na leo tarehe mbili"amesema Nyengela

Dkt.Nyengela amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa bila kupata vipimo sahihi vya wataalamu wa afya kwa kuwa inasababisha wengi wao kuathirika kutokana na kutumia dawa zisizo sahihi.

"Watu wengi wanakumbwa na changamoto halafu wanaenda kununua dawa bila vipimo kwa hiyo ni vizuri kuchukua vipimo ili kupata matibabu sahihi"ameongeza Dkt.Nyengela

Baadhi ya wananchi akiwemo Onesmo Ngimbuchi,Lupeta Mlelwa na Eva Mhala ambao wamejitokeza kupata vipimo hivyo wameshukuru uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuja na zoezi la kutoa vipimo bure kwani wengi wao wamekuwa wakishindwa kupima afya zao kutokana na kukosa fedha.

"Wengi tulikuwa tunashindwa kumuda badhi ya vipimo kwa hiyo tulivyoona hii fursa tumeona ndio nafasi ya kuitumia"wamesema wanufaika

Kanisa Katholiki Duniani huadhimisha Jubilei ya Ukristo kila baada ya miaka 25 ikiwa ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi,Upatanisho na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya kitubio.

Share To:

Post A Comment: