Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuendesha zoezi la Samia Ardhi Kliniki linalofanyika nchi nzima.
Mhe. Senyamule ametoa pongezi hizo leo Machi 5, 2026 alipotembelea kliniki hiyo inayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma.
“Nimekaa sijawahi kuona ubunifu wa jambo hili, na nimeambiwa linafanyika nchi nzima ya Tanzania. Hiki ni kitu cha pekee sana,” amesema Senyamule.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma, awali aliposikia kuhusu kliniki hiyo alijiuliza kama kutapatikana wanawake wa kutosha kwenda kutatuliwa kero zao za ardhi, lakini hali imekuwa tofauti.
“Nilijiuliza kama wanawake watapatikana kwa wingi, lakini leo nimeshangaa kuona na kushuhudia kuwa sasa wanawake wengi wanamiliki ardhi,” amesema Senyamule.
Aidha, amesema kuwa kama jambo hilo lingefanyika miaka kumi au ishirini iliyopita, isingekuwa rahisi kupata wanawake wengi kwa sababu wengi hawakuwa na uelewa wa haki yao ya kumiliki ardhi.
“Kama ungelifanya jambo hili miaka kumi au ishirini iliyopita na kusema wanawake waje washughulikie kero zao za ardhi na kupata hati, usingewapata wengi kwa sababu wakati huo hatukuwa na uelewa kuwa sisi pia tunastahili kumiliki ardhi,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Senyamule amewaasa wanawake kutunza vizuri hati zao za ardhi, akieleza kuwa ardhi ya Dodoma ina thamani kubwa inayoongezeka kila siku.
“Ukishapata hati yako, itunze vizuri kwa sababu ardhi ya Dodoma ina thamani kubwa na thamani yake inaendelea kuongezeka kila siku,” amesema.
Sambamba na hilo, Mhe. Senyamule pia amekabidhi hati miliki kwa baadhi ya wanawake waliofika katika kliniki hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma.
Samia Ardhi Kliniki ilianza rasmi tarehe 2 Machi 2026 katika mikoa yote nchini na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 7 Machi 2026 yenye Kauli Mbiu, Mwanamke; Haki Yako, Miliki Ardhi sasa.


Post A Comment: