‎Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, amefungua mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kuwajengea uelewa wataalamu wa TARURA kutoka TAMISEMI, ofisi ya Makao Makuu, Mikoa, Wilaya, Mhandisi Mshauri pamoja na Mkandarasi katika kutekeleza mradi wa Sanifu na Jenga wa barabara zinazoingia uwanja wa AFCON jijini Arusha.

‎Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhandisi Seff alisema lengo kuu ni kujenga uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya sanifu na jenga ili kuimarisha uzingatiaji wa taratibu, kushughulikia changamoto kwa wakati na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio.

‎Alifafanua kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuzingatia misingi ya usalama, masuala ya kijamii na kimazingira, muda, gharama, thamani, ubora pamoja na mahitaji ya kiutendaji.

‎Mhandisi Seff alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa TARURA, Wakala huo haujawahi kupata mradi mkubwa kama huo, hivyo mafunzo hayo ni fursa muhimu ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ili wawe tayari kushughulikia miradi mikubwa zaidi ijayo.

‎Aliwataka washiriki wa mafunzo kujifunza kwa umakini na kuuliza maswali yatakayowaongezea uelewa, akisisitiza kuwa jukumu walilonalo ni kubwa na linahitaji umakini wa hali ya juu katika kila hatua ya utekelezaji.

‎Aidha, aliwakumbusha wasimamizi wa mradi kuzingatia muda akieleza kuwa barabara hizo zinatakiwa kukamilika ifikapo Mei 2027 bila nyongeza ya muda.

‎“Serikali imeiamini TARURA kwa kuipatia jukumu hilo kwa manufaa ya Taifa hivyo hamna budi kufanya kazi usiku na mchana”.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: