‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imewakutanisha wahandisi na wataalamu wa sekta ya barabara katika mafunzo maalum yanayolenga kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara wakati wa usanifu, ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara nchini.

‎Mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Morogoro yanalenga kuongeza uelewa na uwezo wa wataalamu katika kuzingatia viwango vya usalama barabarani ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.

‎Akizungumza katika mahojiano maalum, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa RISE, Mhandisi Lwitiko Mwandobo, amesema mafunzo hayo yameandaliwa mahsusi kuwajengea uwezo wahandisi na kuwakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara unazingatiwa tangu hatua ya usanifu hadi utekelezaji wa miradi.

‎"Tunataka kuhakikisha kwamba kila mradi wa barabara unazingatia usalama kwa kuweka alama zote muhimu, miundombinu rafiki kwa watumiaji na hatua nyingine za kinga zitakazosaidia kupunguza ajali zinazoweza kuepukika. Hii ni sehemu ya juhudi za kulinda maisha ya wananchi na mali zao", amesema Mhandisi Mwandobo.

‎Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga amesema usalama wa watumiaji wa barabara ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kufikia lengo la kupunguza kwa kiwango kikubwa ajali za barabarani na pia kuna umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya barabara.

‎"Tukizingatia usalama katika kila hatua ya ujenzi wa barabara, kuimarisha elimu kwa umma na kuhakikisha miundombinu inakidhi viwango vinavyotakiwa, tutapunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani na madhara yake kwa jamii",  amesema Mhandisi Mkinga.

‎Naye, Mratibu wa Masuala ya Usalama Barabarani kutoka (TARURA), Mhandisi Faizer Mbange, amesema mwelekeo wa sasa katika ujenzi wa barabara unalenga kuhakikisha mahitaji ya makundi yote ya watumiaji wa barabara yanazingatiwa ikiwemo waenda kwa miguu, waendesha baiskeli, bodaboda, bajaji pamoja na watumiaji wa vyombo vingine vya usafiri.

‎Amesema tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo usanifu wa barabara ulijikita zaidi katika magari, sasa miundombinu ya barabara inapaswa kuwa jumuishi na salama kwa kila mtumiaji bila kujali aina ya usafiri anaotumia.

‎Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za sekta ya barabara na usafiri zikiwemo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Ofisi ya Waziri Mkuu– TAMISEMI, TARURA na Mfuko wa Barabara (Road Fund).






Share To:

Post A Comment: