
Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wameonesha moyo wa kujitolea kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye matatizo ya moyo wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo, kwa niaba ya MWENYEKITI wa Kamati ya wanawake TTCL, Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi. Adeline Berchimance,amesema wanawake wa shirika hilo wameguswa na changamoto zinazowakabili watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na wazazi na walezi wao.
Amesema wameona umuhimu wa kufika katika taasisi hiyo ili kuwafariji na kuwapa matumaini watoto pamoja na familia zao katika kipindi wanachopitia cha matibabu.
“Watoto hawa ni sehemu ya jamii yetu na wana haki ya kupata upendo, faraja na msaada kutoka kwa watu wanaowazunguka. Hivyo tumeona ni muhimu kuwafikia na kuwapa msaada huu mdogo kama ishara ya upendo wetu,” amesema Bi. Adeline.
Ameeleza kuwa msaada uliotolewa umejumuisha pampas kwa watoto, maziwa kwa watoto wachanga pamoja na pedi kwa wazazi na walezi wanaokaa hospitalini kwa muda mrefu wakihudumia watoto wao.
Amesema wanawake wa TTCL wanaamini kuwa pamoja na msaada wa vifaa, uwepo wao hospitalini hapo unatoa faraja na kuongeza matumaini kwa watoto pamoja na wazazi wao.






Post A Comment: