Na Mwandishi Wetu, Lusaka
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unashiriki Kongamano la Kimataifa la Nishati Endelevu ya Kuni na Mkaa (Sustainable Woodfuel Forum) linaloendelea Lusaka, Zambia, likiwa jukwaa la kimataifa la kubadilishana uzoefu na mbinu bora za usimamizi wa misitu na nishati ya miti.
Kongamano hilo linafanyika chini ya Programu ya Dryland Sustainable Landscapes Impact Programme (DSL-IP) kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kuratibiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Serikali ya Zambia.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mhifadhi Mkuu TFS, Kassim Ally, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya azma ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Ally amesema juhudi hizo zinajumuisha utekelezaji wa sera, uwekezaji katika nishati mbadala na kampeni za elimu kwa umma ili kubadilisha tabia ya matumizi ya nishati.
Ameeleza kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza ukataji miti hovyo, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi dhidi ya athari za moshi wa majumbani.
Kwa mujibu wa Ally, ushiriki wa TFS unafanyika kupitia mradi wa Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania unaolenga kurejesha mifumo ikolojia na kupunguza upotevu wa bioanuwai.
Amesema mradi huo pia unalenga kuimarisha ustahimilivu wa uzalishaji katika maeneo ya Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame katika Mkoa wa Tabora (Wilaya za Kaliua, Sikonge na Urambo) na Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, jamii zinashirikishwa moja kwa moja katika uhifadhi huku zikipewa fursa za kunufaika kiuchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali.
Kongamano hilo linawakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali za ukanda wa Miombo-Mopane kujadili mahitaji ya nishati ya kuni na mkaa hadi mwaka 2050 na athari zake kwa uchumi na mazingira.
Katika maonesho yanayoambatana na kongamano hilo, TFS imewasilisha teknolojia za nishati safi ya kupikia na mbinu mbadala za matumizi ya kuni na mkaa.

Post A Comment: