Articles by "TFS"
Showing posts with label TFS. Show all posts

 

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unatarajia kujenga kiwanda kipya na uwekaji mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuchakata mazao ya nyuki ili kuwezesha kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi la asali.

Kiwanda hicho kipya kitajengwa wilayani Manyoni, Mkoa wa  Singida ambako kuna kiwanda kidogo cha uchakataji kinachohudumia Kanda ya Kati inayojumisha mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma ambacho kinatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh milioni 200 .

Mhifadhi Mkuu Daraja la Pili wa TFS , Claudia Kinabo amesema hayo alipozungumzia mikakati ya uzalishaji wa mazao ya nyuki ikiwemo asali katika kanda hiyo na namna ilivyojioanga kwenye maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani Mei 20 mwaka huu ambapo kitaifa ya kifanyika mkoani Tabora.

Kinabo ambaye ni msimamizi wa kitengo cha Ufugaji Nyuki Kanda ya Kati alisema Wakala huo umetenga bajeti kwa ajili ya kujenga kiwanda kikubwa zaidi ya ukataji wa mazao ya nyuki ambapo kwa sasa kipo kiwanda kidogo katika kituo cha Wilaya ya Manyoni.

“Ujenzi kwa maana ya upanuzi huu wa kiwanda cha Manyoni utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza sekta ya asali na kuongeza uzalishaji katika eneo hili,” amesema Kinabo.

Kinabo amesema Kanda  yaKati unaendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa asali chini ya TFS kwa sababu ina mazingira mazuri ya misitu yanayofaa kwa ufugaji nyuki.

Amesema kuwa Kanda hiyo una mashamba makubwa matano ya nyuki yaliyopo katika wilaya za Singida na Kondoa, maeneo yanayojulikana kwa mazingira mazuri ya ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali bora.

Naye, Mhifadhi Nyuki Shamba la Nyuki Manyoni, Mrina Robert amesema kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kimekuwa kikichakata mazao hayo kutoka wilaya mbalimbali za Kanda ya Kati pamoja na asali za wadau mbalimbali .

Mrina amesema kiwanda cha sasa licha ya kuendelea kuchakata mazao ya nyuki  kikiwa na uwezo wa kuchakata kilo 500 kwa saa nane  kwa siku.

Amesema kutokana na mahitaji makubwa na mtambo uliopo  ni mdogo pamoja na jengo, wakala katika bajeti yake umejipanga kujenga jengo kubwa la kiwanda na kuweka mitambo mikubwa nay a kisasa zaidi  ya kuchakata mazao ya nyuki kwa maana ya asali, nta na mengine.

Mrina amesema kiwanda hicho kipya kitachangia kuongeza kasi ya uchakataji wa asali  na kutoa ushawishi kwa wadau wenye mashamba ya nyuki kuleta mazao yao kuchakatwa.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu na Msaidizi wa Kamanda wa TFS Kanda ya Kati anayeshughulikia Dawati la Mipango na Masoko, Ignas Lupala alisema kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 lengo lilikuwa kuzalisha tani 20 za mazao ya nyuki na hadi kufikia msimu ulipomalizika zilizalishwa tani 16.5 za asali.

Lupala amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Kanda hiyo imeweka lengo la kuvuna jumla ya tani 21 za asali na  bado msimu wa uvunaji unaendelea na mikakati mbalimbali imewekwa ya uzalishaji  mazao ya nyuki kwa wingi yanafikiwa kila mwaka.

 


Na Mwandishi Wetu, Lusaka

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unashiriki Kongamano la Kimataifa la Nishati Endelevu ya Kuni na Mkaa (Sustainable Woodfuel Forum) linaloendelea Lusaka, Zambia, likiwa jukwaa la kimataifa la kubadilishana uzoefu na mbinu bora za usimamizi wa misitu na nishati ya miti.

Kongamano hilo linafanyika chini ya Programu ya Dryland Sustainable Landscapes Impact Programme (DSL-IP) kwa ufadhili wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) na kuratibiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa kushirikiana na Serikali ya Zambia.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mhifadhi Mkuu TFS, Kassim Ally, amesema Tanzania inaendelea kutekeleza mikakati ya kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya azma ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034.

Ally amesema juhudi hizo zinajumuisha utekelezaji wa sera, uwekezaji katika nishati mbadala na kampeni za elimu kwa umma ili kubadilisha tabia ya matumizi ya nishati.

Ameeleza kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza ukataji miti hovyo, kulinda misitu na kuboresha afya za wananchi dhidi ya athari za moshi wa majumbani.

Kwa mujibu wa Ally, ushiriki wa TFS unafanyika kupitia mradi wa Integrated Landscape Management in Dry Miombo Woodlands of Tanzania unaolenga kurejesha mifumo ikolojia na kupunguza upotevu wa bioanuwai.

Amesema mradi huo pia unalenga kuimarisha ustahimilivu wa uzalishaji katika maeneo ya Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame katika Mkoa wa Tabora (Wilaya za Kaliua, Sikonge na Urambo) na Wilaya ya Mlele mkoani Katavi kupitia usimamizi shirikishi wa misitu.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, jamii zinashirikishwa moja kwa moja katika uhifadhi huku zikipewa fursa za kunufaika kiuchumi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali.

Kongamano hilo linawakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali za ukanda wa Miombo-Mopane kujadili mahitaji ya nishati ya kuni na mkaa hadi mwaka 2050 na athari zake kwa uchumi na mazingira.

Katika maonesho yanayoambatana na kongamano hilo, TFS imewasilisha teknolojia za nishati safi ya kupikia na mbinu mbadala za matumizi ya kuni na mkaa.

 Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeingia katika mpango wa ushirikiano na kampuni ya Land Africa Safaris ili kukuza utalii wa ikolojia kupitia tukio la Cape to Cairo Arusha International Marathon linalotarajiwa kufanyika Mei 28 hadi 30, 2026 mkoani Arusha.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichofanyika Machi 17, 2026 katika Ofisi ya Mhifadhi Mkuu wa Ziwa Duluti, Arumeru.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mhifadhi Mkuu wa Ziwa Duluti, Peter A. Myonga, alisema ushirikiano huo ni fursa muhimu kwa TFS kutumia michezo kutangaza vivutio vya misitu na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea maeneo hayo.

Alisema tukio hilo linatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea ongezeko la wageni, muda wa kukaa kwa watalii jijini Arusha na mapato yatokanayo na utalii.

Kwa mujibu wa Myonga, TFS imejipanga kushiriki kikamilifu katika mbio hizo ambapo vivutio vyake vya Napuru na Ziwa Duluti vitatembelewa na washiriki wa mbio hizo kwa ajili ya kutangaza utalii wa misitu na nyuki (api-tourism).

Aidha, alisema washiriki wa mbio hizo watapata fursa ya kutembelea vivutio vya misitu ikiwemo Shamba la Miti Meru na Ziwa Duluti kabla na baada ya tukio, huku mipango ikiwekwa kuhakikisha katika msimu ujao wa 2027 njia ya mbio inapita ndani ya hifadhi hizo ili kuongeza mvuto wa utalii.

Aliongeza kuwa TFS itanufaika pia kwa kuanzisha mabanda ya maonyesho, kutengeneza vifurushi vya utalii, huduma za kambi katika eneo la Napuru na kushiriki katika hafla ya Gala Dinner itakayotoa jukwaa la kuitangaza sekta ya misitu na nyuki.

Kwa upande wake, Haffy Mohamed  kutoka Land Africa Safaris alisema wataendelea kushirikiana na TFS kuhakikisha tukio hilo linakuwa chachu ya kukuza utalii wa michezo nchini.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha sekta ya michezo na utalii ili kuongeza mchango wa rasilimali za asili katika uchumi wa Taifa.







Tanzania, kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), imeungana na nchi nyingine za Afrika katika warsha ya kimataifa iliyojadili mbinu mpya za kupima na kufuatilia kiwango cha hewa ukaa kinachofyonzwa na miti inayoota nje ya misitu, maarufu kama Trees Outside Forests (TOF).

Warsha hiyo ya siku mbili, Desemba 2 hadi 3, 2025 imefanyika katika Hoteli ya Sigelege, Salima nchini Malawi chini ya uratibu wa Michigan State University (MSU), kwa kushirikiana na vyuo na taasisi za utafiti kutoka Malawi, Senegal na Marekani.

Tanzania inawakilishwa na wahifadhi wawili kutoka TFS, Rogers Nyinondi na Jameseth Lazaro, walioalikwa kutokana na nafasi ya TFS kuratibu utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kurejesha uoto wa asili kupitia African Forest Landscape Restoration Initiative (AFR100). Kupitia mpango huo, Tanzania imeahidi kurejesha takribani hekta milioni 5.2 za maeneo yaliyoharibika ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa Mkufunzi Mkuu kutoka Michigan State University (MSU), Prof. David L. Skole, warsha hiyo imetoa hatua kubwa ya kiufundi katika ufuatiliaji wa hewa ukaa kwa kutumia teknolojia za high-resolution satellite remote sensing, deep machine learning na allometric scaling models, mbinu zinazowezesha kutambua na kupima miti mmoja mmoja katika maelfu ya hekta. 

Skole alisema mafunzo hayo, ambayo yamemalizika leo, yamelenga kusaidia nchi wanachama kuimarisha mifumo ya uthibitishaji wa taarifa za urejeshaji mazingira na kuweka msingi thabiti wa usimamizi wa ardhi barani Afrika.

Kwa upande wa Tanzania, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Rogers Nyinondi, alisema ushiriki wa Tanzania umeongeza uelewa wa kitaalamu kuhusu mchango wa miti nje ya misitu, ikiwemo kilimo mseto katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Huku akibainisha kuwa mbinu mpya walizopatiwa zitaboresha ukusanyaji wa takwimu za kaboni, kuimarisha upangaji wa sera na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya urejeshaji ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Warsha hiyo imewaleta pamoja wanasayansi na wataalamu kutoka Rwanda, Kenya, Tanzania, DRC, Senegal, India na Malawi, pamoja na wadau wa AFR100, kujadili maendeleo ya mradi wa kimataifa unaofadhiliwa na MSU.

 


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti la Sao Hill, limeanza kutumia teknolojia mpya za kidigitali kuboresha utambuzi na udhibiti wa matukio ya moto misituni — hatua inayolenga kulinda misitu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa TFS wa kuboresha usimamizi wa misitu kwa kutumia sayansi na ubunifu, sambamba na jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za taifa.

Kwa mujibu wa TFS, teknolojia hizo zinasaidia kutambua kwa haraka eneo lililoathiriwa na moto na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa vikosi vya ulinzi wa misitu ili kuchukua hatua za haraka kabla madhara hayajawa makubwa.

Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Mussa Kitivo, amesema kuwa matumizi ya teknolojia hizo yameanza kuleta matokeo ya wazi, ikiwemo kupungua kwa matukio ya moto na kuongezeka kwa utambuzi wa wahusika wanaosababisha majanga hayo.

“Kwa sasa tunapata taarifa mapema zaidi, na moto unadhibitiwa kabla haujasambaa. Hii imepunguza sana uharibifu wa hekta za misitu na kuokoa miti mingi ambayo ingepotea,” alisema Kitivo.

Ameongeza kuwa mfumo huo unawawezesha watumishi wa misitu na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kutoa taarifa za matukio ya moto kwa wakati kupitia njia za kidigitali.

TFS imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu matumizi ya vifaa hivyo vya kisasa pamoja na uchambuzi wa taarifa zinazokusanywa, ili kuongeza ufanisi katika kulinda misitu.

Mtaalamu wa mifumo hiyo, Bashily Njollah Msangi, alisema teknolojia hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha misitu inalindwa kwa usahihi na kasi inayohitajika.

“Teknolojia hizi zinasaidia si tu kugundua moto, bali pia kubaini ni nani aliyehusika. Hii ni hatua kubwa katika kulinda misitu yetu. Tunawahimiza wananchi waone teknolojia kama rafiki katika uhifadhi,” alisema Msangi.

TFS–Sao Hill imetoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na wahifadhi kwa kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili za moto, na kuepuka matumizi holela ya moto hasa katika shughuli za kilimo na uwindaji.

Kupitia mkakati huu, TFS–Sao Hill imejidhihirisha kama taasisi inayoendana na mageuzi ya teknolojia duniani, ikiimarisha juhudi za taifa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha misitu inabaki salama kwa vizazi vijavyo.

“Matumizi ya teknolojia ni silaha mpya katika kulinda misitu ya Tanzania,” amesema Kitivo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mapambano ya kudhibiti moto misituni.











 

Shamba la Miti Sao Hill, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), limefanya ukaguzi wa utekelezaji wa kazi kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha mpango kazi unatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa kwa wakati.

Katika ukaguzi huo, maeneo yaliyotathminiwa ni pamoja na bustani na vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa upandaji, ujenzi wa barabara za kinga moto kwa kudhibiti matukio ya moto, usafishaji wa mashamba ya miti, pamoja na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na mazao ya misitu.

Vilevile, timu ya tathmini ilipitia vitengo mbalimbali vya Shamba la Sao Hill, ikiwemo Uvunaji na Leseni, Utawala, Ulinzi wa Msitu, Ugani na Uenezi, Utalii, Ujenzi na Barabara, Karakana, pamoja na shughuli za ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yake.

Katika mapendekezo yake, wahifadhi walihimiza mpango kazi wa mwaka ufuatwe kikamilifu ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa kwa wakati. Pia, walisisitiza kuongeza ushirikiano kati ya shamba na wananchi wanaolizunguka ili kuimarisha juhudi za uhifadhi wa misitu.

Aidha, suala la moto liliibuliwa kama changamoto kubwa, ikibainishwa kuwa limekuwa likisababisha hasara kwa misitu ya serikali na wananchi kutokana na shughuli za kijamii zinazotumia moto bila tahadhari. 

Hivyo, elimu ya udhibiti wa moto iliagizwa kuendelezwa sambamba na hatua za haraka kuchukuliwa pale viashiria vya hatari vinapojitokeza.

Wahifadhi pia walikumbushwa kuongeza ubunifu na bidii katika utendaji wao wa kila siku, ili kuhakikisha mpango kazi wa mwaka mzima unakamilishwa kwa ufanisi na kwa wakati.















Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuweka mikakati ya kujenga uwezo kwa wahifadhi wake ili kuboresha usimamizi wa misitu kwa kuwatambua mapema viashiria hatarishi mahala pa kazi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Agosti 22, 2025 katika Shamba la Miti Sao Hill, yametolewa na Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Ernest Mwasalwiba, kwa lengo la kuwajengea uwezo wahifadhi kuhusu namna ya kuzuia changamoto zinazoweza kudhoofisha utendaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Mwasalwiba alisema ni muhimu kwa watumishi wa umma, hususan wahifadhi, kufahamu viashiria vinavyoweza kusababisha madhara kwa taasisi na taifa, ikiwemo moto wa misitu, rushwa, utoaji wa huduma duni, pamoja na uvujaji wa siri za serikali.

“Kama tunavyoona kwa TFS, viashiria hatarishi ni pamoja na matukio ya moto misituni yanayosababisha hasara kubwa. Kila mmoja anapaswa kuhakikisha anavitambua mapema na kuchukua hatua stahiki ili kulinda misitu na kuimarisha utendaji,” alisema Dk. Mwasalwiba.

Aliongeza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea, jambo linalopelekea kushindwa kugundua mapema viashiria hatarishi na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa taasisi na jamii.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ubunifu, uadilifu na weledi katika utendaji wa kila siku, akibainisha kuwa ni nyenzo za kujenga taswira nzuri ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu anayesimamia Mipango, Masoko na Matumizi wa Shamba la Miti Sao Hill, SCO Peter Nyahende, alisema wanamshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, kwa kuwezesha mafunzo hayo ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiongeza uelewa wa watumishi katika kazi zao.

“Tutaendelea kutumia mafunzo haya kuongeza ubunifu na ufanisi ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa,” alisema Nyahende.







 

Mamia ya wananchi wamejitokeza katika banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupata huduma mbalimbali za kielimu na kiafya wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayoendelea jijini Dodoma.

Miongoni mwa vivutio vikubwa katika banda hilo lililoko viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), ni huduma ya tiba ya kuimarisha kinga ya mwili kwa kutumia nyuki (api-therapy), iliyokuwa ikitolewa na Mhifadhi Brenda Mwakipesile kutoka TFS.

Mwakipesile alisema tiba hiyo ya asili inasaidia kuchochea kinga ya mwili na kutoa ahueni kwa baadhi ya maumivu ya muda mrefu, hasa ya viungo.

“Tiba hii inatumia sumu ya nyuki kwa njia salama na inayodhibitiwa, na imekuwa na matokeo chanya kwa baadhi ya wagonjwa waliowahi kuipokea. Leo tumeona muitikio mkubwa wa wananchi walio na shauku ya kujifunza na kupata huduma hii,” alisema.

Mbali na huduma hiyo, TFS ilitoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa misitu, matumizi ya nishati safi ya kupikia, uzalishaji wa mkaa mbadala, upandaji wa miti na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Maonesho haya yamebeba kaulimbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti Matumizi ya Plastiki”, yakihusisha taasisi mbalimbali za Serikali, mashirika ya kimataifa, sekta binafsi na wananchi.
Wananchi waliotembelea banda la TFS walionesha kufurahishwa na huduma na elimu waliyoipata, wakieleza kuwa ni tofauti na ilivyozoeleka katika maonyesho mengine.

“Nimejifunza mengi kuhusu misitu, lakini pia sikuwahi kufikiria nyuki wanaweza kutumika kama tiba. Ni jambo jipya na la kuvutia sana,” alisema Rehema John, mkazi wa Dodoma.

Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira yanatarajiwa kufikia kilele chake Juni 5, yakilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa Taifa.



Uzinduzi wa West Kili Forest Tour Challenge 2025 umefanyika rasmi mei 23,2025 lengo kuu likuwa ni kuinua Utalii Endelevu na Uchumi wa Kijani,kutangaza utalii wa ikolojia,vivutio vilivyopo na kutoa elimu ya uhifadhi kwa vitendo pamoja na kuona fursa zanuweiezaji ndani ya hifadhi ya shamba la Miti West Kilimanjaro.


Akizungumza wakati akitoa salamu kwa mgeni rasmi,wadau wa mazingira, wawakilishi wa sekta ya utalii, wananchi na waandishi wa habari, Mhifadhi mkuu Hifadhi ya Msitu West Kilimanjaro PCO. Robert Faida, alisema kuwa hiyo ni fursa ya pekee kuwakutanisha wadau wa utalii na kutengeneza mtandao wa biashara, kukuza utalii na uchumi

Aidha PCO Faida amesema tukio la mwaka huu linatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 2,000 na kuweka West Kilimanjaro kwenye ramani ya Kimataifa ya utalii wa Mazingira hivyo TFS iliona ni vyema kutumia vivutio hivyo vya utalii kutangaza utalii, ambapo amewakaribisha Sekta binafsi kushirikiana na TFS katika kuendeleza eneo hilo.

"Hapa washiriki wanapata elimu kwa vitendo na kuona umuhimu wa uhifadhi kwani nieneo la kimkakati na shindani hivyo itatusaidia kutangaza fursa za uwekezaji zinazoweza kufanyika ndani ya hifadhi, kwa uwepo kwa mlima Kilimanjaro na root ya Lemotsho, wageni wengi wanaigia, vile vile washiriki wetu wa mbio hizi wanakutana na kutengeneza mtandao wa kibiashara "Alisema Faida.

Akizungumza Mgeni rasmi katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka,amesema msimu huo wa tano wa West Kili Forest Tour Challenge 2025, ni tukio

kubwa linalotarajiwa kufanyika tarehe 21 hadi 22 Juni 2025 katika misitu ya West Kilimanjaro, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro.

Dkt. Timbuka alieleza kuwa lengo la tukio hilo ni kukuza utalii endelevu,uhifadhi elimu, uwekezaji na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kuwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kushirikiana katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, amewahimiza wananchi kinjtokeza kwa wingi kushiriki kwani kuna manufaa ya moja kwa moja kwa jamii, siyo tu katika nyanja ya uchumi,

"Tukio hili tunatarajia kuwa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali zitakazofanyika ndani ya hifadhi, zikiwemo matembezi na mbio za umbali wa kilomita 21,10 na 5 kwa ajili ya kujionea mandhari ya kipekee ya misitu ya West Kilimanjaro; mbio za baiskeli na moto-cross; maonyesho ya mavazi ya asili, michezo ya watoto, pamoja na ngoma na sanaa za jadi. Alisema Dkt Timbuka.

Amesema usajili wa washiriki wa mwaka huu umerahisishwa kwa njia mbili kuu: moja ni kupitia mtandao kwa kutembelea tovuti rasmi ya www.westkili.co.tz au tickets.westkili.co.tz, na nyingine ni kwa kufanya malipo ya moja kwa moja kwa simu kupitia namba ya Tigo 7878284 kwa jina West Kili Run and Bike au M-Pesa 5362338 kwa jina Pedal Tz.

Azungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo,Mhifadhi Mwandamizi, Tulizo Kilaga alisema kuwa West Kili Challenge inaakisi mkakati wa TFS wa kutumia misitu kama kichocheo cha uchumi, na kuongeza kuwa tukio hili linaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza uchumi wa kijani na kuhakikisha misitu inanufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

"Mhe. Mkuu wa wilaya Prof anatambua kazi kubwa inayofanywa katika wilaya yako katika promotion ya utalii ameniambia nikwambie kwa mwaka huu TFS imevunja rekodi katika mapato ya utalii ambapo tumefika zaidi ya Bil 2 na huku West Kilimanjaro ni kituo kinachoongoza kwa mapato ya TFS. Alisema Kilaga.

"Tunapotangaza ‘Explore Life in Nature,’ tunawaalika Watanzania kuiona TFS ni fursa pia zaidi ya kuni,mkaa, mbao,tumetoka huko utalii wa mazingira umeshika chati na unsingiza maps to kwa kiasi kikubwa,alisema Kilaga.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka,akizindua rasmi. msimu wa tano wa West Kili Forest Tour Challenge 2025, ndani ya Hifadhi shamba la Miti West Kilimanjaro