Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti la Sao Hill, limeanza kutumia teknolojia mpya za kidigitali kuboresha utambuzi na udhibiti wa matukio ya moto misituni — hatua inayolenga kulinda misitu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa TFS wa kuboresha usimamizi wa misitu kwa kutumia sayansi na ubunifu, sambamba na jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za taifa.

Kwa mujibu wa TFS, teknolojia hizo zinasaidia kutambua kwa haraka eneo lililoathiriwa na moto na kurahisisha utoaji wa taarifa kwa vikosi vya ulinzi wa misitu ili kuchukua hatua za haraka kabla madhara hayajawa makubwa.

Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Mussa Kitivo, amesema kuwa matumizi ya teknolojia hizo yameanza kuleta matokeo ya wazi, ikiwemo kupungua kwa matukio ya moto na kuongezeka kwa utambuzi wa wahusika wanaosababisha majanga hayo.

“Kwa sasa tunapata taarifa mapema zaidi, na moto unadhibitiwa kabla haujasambaa. Hii imepunguza sana uharibifu wa hekta za misitu na kuokoa miti mingi ambayo ingepotea,” alisema Kitivo.

Ameongeza kuwa mfumo huo unawawezesha watumishi wa misitu na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi kutoa taarifa za matukio ya moto kwa wakati kupitia njia za kidigitali.

TFS imeendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu matumizi ya vifaa hivyo vya kisasa pamoja na uchambuzi wa taarifa zinazokusanywa, ili kuongeza ufanisi katika kulinda misitu.

Mtaalamu wa mifumo hiyo, Bashily Njollah Msangi, alisema teknolojia hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha misitu inalindwa kwa usahihi na kasi inayohitajika.

“Teknolojia hizi zinasaidia si tu kugundua moto, bali pia kubaini ni nani aliyehusika. Hii ni hatua kubwa katika kulinda misitu yetu. Tunawahimiza wananchi waone teknolojia kama rafiki katika uhifadhi,” alisema Msangi.

TFS–Sao Hill imetoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na wahifadhi kwa kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili za moto, na kuepuka matumizi holela ya moto hasa katika shughuli za kilimo na uwindaji.

Kupitia mkakati huu, TFS–Sao Hill imejidhihirisha kama taasisi inayoendana na mageuzi ya teknolojia duniani, ikiimarisha juhudi za taifa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha misitu inabaki salama kwa vizazi vijavyo.

“Matumizi ya teknolojia ni silaha mpya katika kulinda misitu ya Tanzania,” amesema Kitivo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika mapambano ya kudhibiti moto misituni.











Share To:

Post A Comment: