Shamba la Miti Sao Hill, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), limefanya ukaguzi wa utekelezaji wa kazi kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha mpango kazi unatekelezwa kwa ufanisi na changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa kwa wakati.

Katika ukaguzi huo, maeneo yaliyotathminiwa ni pamoja na bustani na vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa upandaji, ujenzi wa barabara za kinga moto kwa kudhibiti matukio ya moto, usafishaji wa mashamba ya miti, pamoja na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na mazao ya misitu.

Vilevile, timu ya tathmini ilipitia vitengo mbalimbali vya Shamba la Sao Hill, ikiwemo Uvunaji na Leseni, Utawala, Ulinzi wa Msitu, Ugani na Uenezi, Utalii, Ujenzi na Barabara, Karakana, pamoja na shughuli za ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yake.

Katika mapendekezo yake, wahifadhi walihimiza mpango kazi wa mwaka ufuatwe kikamilifu ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa kwa wakati. Pia, walisisitiza kuongeza ushirikiano kati ya shamba na wananchi wanaolizunguka ili kuimarisha juhudi za uhifadhi wa misitu.

Aidha, suala la moto liliibuliwa kama changamoto kubwa, ikibainishwa kuwa limekuwa likisababisha hasara kwa misitu ya serikali na wananchi kutokana na shughuli za kijamii zinazotumia moto bila tahadhari. 

Hivyo, elimu ya udhibiti wa moto iliagizwa kuendelezwa sambamba na hatua za haraka kuchukuliwa pale viashiria vya hatari vinapojitokeza.

Wahifadhi pia walikumbushwa kuongeza ubunifu na bidii katika utendaji wao wa kila siku, ili kuhakikisha mpango kazi wa mwaka mzima unakamilishwa kwa ufanisi na kwa wakati.















Share To:

Post A Comment: