Tanzania, kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), imeungana na nchi nyingine za Afrika katika warsha ya kimataifa iliyojadili mbinu mpya za kupima na kufuatilia kiwango cha hewa ukaa kinachofyonzwa na miti inayoota nje ya misitu, maarufu kama Trees Outside Forests (TOF).

Warsha hiyo ya siku mbili, Desemba 2 hadi 3, 2025 imefanyika katika Hoteli ya Sigelege, Salima nchini Malawi chini ya uratibu wa Michigan State University (MSU), kwa kushirikiana na vyuo na taasisi za utafiti kutoka Malawi, Senegal na Marekani.

Tanzania inawakilishwa na wahifadhi wawili kutoka TFS, Rogers Nyinondi na Jameseth Lazaro, walioalikwa kutokana na nafasi ya TFS kuratibu utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kurejesha uoto wa asili kupitia African Forest Landscape Restoration Initiative (AFR100). Kupitia mpango huo, Tanzania imeahidi kurejesha takribani hekta milioni 5.2 za maeneo yaliyoharibika ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa Mkufunzi Mkuu kutoka Michigan State University (MSU), Prof. David L. Skole, warsha hiyo imetoa hatua kubwa ya kiufundi katika ufuatiliaji wa hewa ukaa kwa kutumia teknolojia za high-resolution satellite remote sensing, deep machine learning na allometric scaling models, mbinu zinazowezesha kutambua na kupima miti mmoja mmoja katika maelfu ya hekta. 

Skole alisema mafunzo hayo, ambayo yamemalizika leo, yamelenga kusaidia nchi wanachama kuimarisha mifumo ya uthibitishaji wa taarifa za urejeshaji mazingira na kuweka msingi thabiti wa usimamizi wa ardhi barani Afrika.

Kwa upande wa Tanzania, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Rogers Nyinondi, alisema ushiriki wa Tanzania umeongeza uelewa wa kitaalamu kuhusu mchango wa miti nje ya misitu, ikiwemo kilimo mseto katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. Huku akibainisha kuwa mbinu mpya walizopatiwa zitaboresha ukusanyaji wa takwimu za kaboni, kuimarisha upangaji wa sera na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya urejeshaji ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.

Warsha hiyo imewaleta pamoja wanasayansi na wataalamu kutoka Rwanda, Kenya, Tanzania, DRC, Senegal, India na Malawi, pamoja na wadau wa AFR100, kujadili maendeleo ya mradi wa kimataifa unaofadhiliwa na MSU.

Share To:

Post A Comment: