Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuweka mikakati ya kujenga uwezo kwa wahifadhi wake ili kuboresha usimamizi wa misitu kwa kuwatambua mapema viashiria hatarishi mahala pa kazi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo, Agosti 22, 2025 katika Shamba la Miti Sao Hill, yametolewa na Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Ernest Mwasalwiba, kwa lengo la kuwajengea uwezo wahifadhi kuhusu namna ya kuzuia changamoto zinazoweza kudhoofisha utendaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk. Mwasalwiba alisema ni muhimu kwa watumishi wa umma, hususan wahifadhi, kufahamu viashiria vinavyoweza kusababisha madhara kwa taasisi na taifa, ikiwemo moto wa misitu, rushwa, utoaji wa huduma duni, pamoja na uvujaji wa siri za serikali.

“Kama tunavyoona kwa TFS, viashiria hatarishi ni pamoja na matukio ya moto misituni yanayosababisha hasara kubwa. Kila mmoja anapaswa kuhakikisha anavitambua mapema na kuchukua hatua stahiki ili kulinda misitu na kuimarisha utendaji,” alisema Dk. Mwasalwiba.

Aliongeza kuwa changamoto kubwa ni baadhi ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea, jambo linalopelekea kushindwa kugundua mapema viashiria hatarishi na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa taasisi na jamii.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ubunifu, uadilifu na weledi katika utendaji wa kila siku, akibainisha kuwa ni nyenzo za kujenga taswira nzuri ya taasisi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu anayesimamia Mipango, Masoko na Matumizi wa Shamba la Miti Sao Hill, SCO Peter Nyahende, alisema wanamshukuru Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, kwa kuwezesha mafunzo hayo ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiongeza uelewa wa watumishi katika kazi zao.

“Tutaendelea kutumia mafunzo haya kuongeza ubunifu na ufanisi ili kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa,” alisema Nyahende.







Share To:

Post A Comment: