Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Selian imetumia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi kuonesha dhamira yake ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuongeza ufanisi wa kazi kwa kushirikiana kwa karibu na rasilimali watu wake.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa hamasa kubwa jijini Arusha, Mkurugenzi wa TARI Selian, Dkt. Karesma Joseph Chuwa, alisema kuwa taasisi hiyo inatambua umuhimu wa wafanyakazi kama mhimili wa mafanikio ya taasisi, na hivyo imeweka mkazo mkubwa kwenye mazingira bora ya kazi, ushirikishwaji, na motisha.

"TARI Seliani inashirikiana kwa ukaribua na wafanyakazi  wake tunafanya kazi kama timu ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliojiwekea" alisema

Alibainisha kuwa taasisi hiyo imeendelea kuwekeza katika utafiti wa kisayansi unaolenga kukuza mbegu bora za mazao ya bustani zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kulinda usalama wa chakula na kuongeza tija mashambani.

Aidha, Dkt. Chuwa alieleza kuwa TARI Selian imetambua changamoto ya utapiamlo katika jamii na kwa sasa inafanya tafiti mahsusi za kuzalisha mbegu zenye virutubisho vya kutosha ili kuhakikisha lishe bora kwa jamii, hususan wanawake wajawazito na watoto.

“Mbegu zenye virutubisho ni suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto ya lishe. Tunataka kuona wakulima wakiingiza kipato, lakini pia familia zao zikifaidi lishe bora kutoka kwenye mazao yanayozalishwa,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Dkt. Chuwa, TARI Selian kwa sasa inahudumia Kanda ya Kaskazini kwa ubora wa hali ya juu, na tayari imewafikia zaidi ya wakulima milioni mbili nchini kupitia programu mbalimbali za mafunzo, huduma za ugani na usambazaji wa teknolojia za kisasa za kilimo.

Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa muhimu kwa TARI Selian kuonyesha mafanikio yake na kuendelea kujenga mahusiano imara na wafanyakazi wake kama njia ya kufanikisha lengo kuu la kuchochea maendeleo endelevu kupitia utafiti bora wa kilimo bora.





Share To:

Post A Comment: