Kuanzishwa kwa Kampasi ya Njombe ya Chuo Kikuu cha Dodoma kupitia Mradi wa HEET kumeanza kutaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu, ajira na uchumi wa mkoa wa Njombe. Mradi huu unalenga kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Kusini na kuchochea maendeleo ya miundombinu ya kisasa.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, alipokutana na viongozi wa Mkoa wa Njombe akiwemo Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala na Kamati ya Ulinzi na Usalama. Alisema Njombe imepata fursa ya kipekee kwa kuwa na matawi ya vyuo vikuu zaidi ya kimoja.
Prof. Nombo alieleza kuwa uwepo wa kampasi hiyo utachochea shughuli za kiuchumi katika maeneo jirani. Alisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba za makazi, hosteli za wanafunzi, na vituo vya huduma kama maduka na migahawa ili kuandaa mazingira rafiki kwa wanafunzi na watumishi wa kampasi hiyo.
Aliongeza kuwa ongezeko la wanafunzi litahitaji huduma bora za afya, usafi wa mazingira, Miundombinu ya TEHAMA. Alitoa wito kwa taasisi husika kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa wakati katika eneo la Mradi kabla ya kuanza Kwa udahili wa Wanafunzi hasa kwa kuzingatia mfumo wa “blended learning” unaotegemea miundombinu ya intaneti ya uhakika.
Prof. Nombo aliipongeza Njombe kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa miradi ya elimu. Aliahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na mkoa huo kuhakikisha mradi wa Kampasi ya Njombe unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Post A Comment: