Articles by "RCMTAKA"
Showing posts with label RCMTAKA. Show all posts


Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapimwa ili kuweka mazingira mazuri yatakayovutia wawekezaji kuja kuwekeza katika wilaya hiyo na hivyo kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuchochea maendeleo.

Mhe. Mtaka ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Baraza Maalumu la kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Katika kikao hicho, alisisitiza matumizi sahihi ya fedha za umma, uboreshaji wa huduma za jamii pamoja na utekelezaji wa mipango yenye vipaumbele vinavyolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Aidha, Mtaka ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Wangingombe kwa kupata Hati Safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali na kuwataka viongozi kuendelea kusimamia misingi ya sheria na utawala bora. Ameleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi, watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Stephen Nindi, amewahakikishia wananchi na viongozi kuwa wataalamu wataandaa mkakati maalum wa kuhakikisha maeneo yote yanapimwa na kupangwa vizuri ili kuifanya Wanging’ombe kuwa na mpangilio bora wa matumizi ya ardhi, jambo litakalowavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika wilaya hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Agnetha Mpangile, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo yake na kuahidi kuwa halmashauri itaendelea kusimamia kwa umakini ukusanyaji na matumizi ya mapato. Pia ameahidi kuhakikisha watumishi hawakai na fedha mbichi pamoja na kuendeleza ushirikiano na umoja kati ya watumishi na wananchi kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.










Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, amekutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya DL Group, Ndugu Dr. David Langat, pamoja na viongozi wa wafanyabiashara kutoka mkoa wa Njombe.

Katika kikao hicho walihudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali za mkoa, pamoja na vikundi vya uwakilishi kutoka kwa wanawake.

Kikao Hicho Kilijikita  katika kujadili fursa za uwekezaji katika viwanda, na namna ambavyo sekta hii itakavyoinua uchumi wa wananchi wa Njombe. Fursa za uwekezaji zilijikita katika zao la parachichi, chai, na viazi, ambapo kupitia uwekezaji katika viwanda vya usindikaji, kuna matumaini ya kuongeza mnyororo wa dhamani wa mazao haya na kuleta manufaa kwa wakulima na wajasiriamali wa eneo hili.

Mhe. Mtaka alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Njombe, huku akitaja kuwa uwekezaji huu utasaidia kuongeza ajira, kuboresha miundombinu, na kukuza sekta ya kilimo. Wadau walieleza matumaini yao kwamba hatua hizi zitakuza uchumi wa mkoa na kuboresha hali ya maisha ya wakazi wake.













Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ametembelea hospitali mpya ya Mtewele iliyopo katika eneo la Block X, Njombe Mjini, na kushuhudia uwekezaji mkubwa uliotekelezwa na Mzee Philemoni Mtewele.

Katika mazungumzo na Mzee Philemoni Mtewele, Mhe. Mtaka amempongeza kwa kuamua kuwekeza mradi mkubwa nyumbani Njombe, akibainisha kuwa kukamilika kwa hospitali hii kutawawezesha wananchi wa Mkoa wa Njombe na hata wale kutoka maeneo mengine kupata huduma bora za afya kwa urahisi. “Hii ni hatua muhimu inayoongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi na inaonyesha jitihada za kweli za maendeleo,” alisema Mhe. Mtaka.

Kwa upande wake, Mzee Mtewele alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa hospitali na kuonyesha ushirikiano katika kuhakikisha jitihada za kuboresha sekta ya afya zinathaminiwa na serikali pamoja na wananchi.

Hospitali ya Mtewele ni mradi mkubwa wa kimfumo unaoashiria maendeleo katika sekta ya afya, huku ikitoa matumaini makubwa kwa wananchi wa Njombe kupata huduma za matibabu za kisasa na kwa gharama nafuu.













 


Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb), amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Makambako na Wanging’ombe.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, alimkaribisha rasmi na kumshukuru kwa uamuzi wa kufika binafsi kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi. Alisisitiza kuwa ofisi ya mkoa iko tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliopangwa.

Miradi hiyo inatekelezwa chini ya Mradi wa Miji 28, ambao unalenga kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa miji nchini. Kwa upande wa Njombe, zaidi ya shilingi bilioni 80 tayari zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi hiyo, kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.

Akizungumza na viongozi na wataalamu wa maji, Mhe. Aweso alisisitiza kuwa fedha zipo, hivyo hakuna sababu ya ucheleweshaji. Aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora wa hali ya juu kabla ya Desemba 2025, muda uliopangwa kwa maeneo ya Njombe na Makambako.

“Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mkandarasi atakayeshindwa kutimiza wajibu wake,” alisisitiza Waziri Aweso.

Ziara hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na kuendeleza jitihada za kumtua mama ndoo kichwani.