Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso (Mb), amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya maji katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Makambako na Wanging’ombe.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, alimkaribisha rasmi na kumshukuru kwa uamuzi wa kufika binafsi kujionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi. Alisisitiza kuwa ofisi ya mkoa iko tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na ndani ya muda uliopangwa.
Miradi hiyo inatekelezwa chini ya Mradi wa Miji 28, ambao unalenga kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa miji nchini. Kwa upande wa Njombe, zaidi ya shilingi bilioni 80 tayari zimetolewa na serikali kwa ajili ya miradi hiyo, kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India.
Akizungumza na viongozi na wataalamu wa maji, Mhe. Aweso alisisitiza kuwa fedha zipo, hivyo hakuna sababu ya ucheleweshaji. Aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji na kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora wa hali ya juu kabla ya Desemba 2025, muda uliopangwa kwa maeneo ya Njombe na Makambako.
“Ni wajibu wa kila mdau kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mkandarasi atakayeshindwa kutimiza wajibu wake,” alisisitiza Waziri Aweso.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya dhati ya Serikali kuboresha huduma ya maji kwa wananchi na kuendeleza jitihada za kumtua mama ndoo kichwani.
Post A Comment: