Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kuhakikisha maeneo mbalimbali yanapimwa ili kuweka mazingira mazuri yatakayovutia wawekezaji kuja kuwekeza katika wilaya hiyo na hivyo kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuchochea maendeleo.

Mhe. Mtaka ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Baraza Maalumu la kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Katika kikao hicho, alisisitiza matumizi sahihi ya fedha za umma, uboreshaji wa huduma za jamii pamoja na utekelezaji wa mipango yenye vipaumbele vinavyolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Aidha, Mtaka ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Wangingombe kwa kupata Hati Safi ya ukaguzi wa hesabu za serikali na kuwataka viongozi kuendelea kusimamia misingi ya sheria na utawala bora. Ameleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi, watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Stephen Nindi, amewahakikishia wananchi na viongozi kuwa wataalamu wataandaa mkakati maalum wa kuhakikisha maeneo yote yanapimwa na kupangwa vizuri ili kuifanya Wanging’ombe kuwa na mpangilio bora wa matumizi ya ardhi, jambo litakalowavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika wilaya hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Agnetha Mpangile, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo yake na kuahidi kuwa halmashauri itaendelea kusimamia kwa umakini ukusanyaji na matumizi ya mapato. Pia ameahidi kuhakikisha watumishi hawakai na fedha mbichi pamoja na kuendeleza ushirikiano na umoja kati ya watumishi na wananchi kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wilaya hiyo.










Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: