SERIKALI imeendelea kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za kidini nchini katika kuimarisha amani, mshikamano na maendeleo ya taifa.

Amesema hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu leo Juni 19,2026 alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika ibada maalum ya kuliombea Taifa la Tanzania katika kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria Jijini Mwanza.

Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Sangu amesema Serikali inatambua mchango muhimu wa taasisi za kidini katika kujenga jamii yenye maadili mema, umoja na mshikamano, mambo ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya nchi.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo makundi mbalimbali ya kijamii yenye nia njema ya kuijenga Tanzania yetu.

“Tunatambua kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila amani, utulivu, umoja na mshikamano wa wananchi wake”

Katika hatua nyingine Waziri Sangu amewahasa viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, upendo, uvumilivu na maadili mema kwa jamii yetu, hasa kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu.

Vilevile, amewapongeza Umoja wa Unity of Christian International (UCI) kwa kuweka malengo mazuri yanayoendana na Dira ya Taifa 2050 yenye lengo la kujenga jamii yenye mshikamano, upendo, utu na maendeleo.

Kwa upande wake, Askofu Profesa Wilson George Munguza, Askofu kiongozi Unity Christian International Dar es Salaam, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuimarisha umoja na maendeleo ya Taifa.

Ibada hiyo maalum ya kuliombea Taifa viongozi wa dini, waumini na wadau mbalimbali wameshiriki ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuhamasisha amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: