Articles by "KILIMO"
Showing posts with label KILIMO. Show all posts


Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) imeendelea kutoa elimu na kusimamia hatua mbalimbali za kulinda afya ya mimea, kudhibiti visumbufu na kuhakikisha mazao yanayozalishwa na kuingia nchini yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza jijini Tanga katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yanayoendelea kuanzia Oktoba 10 hadi 16, Saumu Zuberi Mwessongo, Afisa Kilimo kutoka TPHPA, Kitengo cha Usafi wa Mimea na Karantini, amesema mamlaka hiyo hukagua mazao yanayoingia na kutoka nchini ili kuzuia kuenea kwa wadudu na magonjwa vamizi ambayo hayapo nchini.


Mwessongo amesema TPHPA hutumia teknolojia mbalimbali, ikiwemo ndege nyuki (drone), kufuatilia mashamba na kubaini maeneo yaliyoathirika na wadudu au magonjwa ya mimea. Aidha, mamlaka hiyo hutoa elimu kwa wakulima kuhusu uchaguzi na matumizi sahihi ya viuatilifu vilivyosajiliwa ili kulinda mazao na afya za walaji.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo pia hutoa vibali vya usafi wa mimea kwa mazao yanayoingizwa nchini na yale yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi. Amesema kupitia ukaguzi wa shehena za mazao, TPHPA huchukua hatua za kuzuia kuingia nchini kwa mazao yaliyobainika kuwa na wadudu au magonjwa vamizi, huku ikitoa maelekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa pale changamoto zinapobainika.


Kwa upande wake, Letan Kurenia Mollel, mtaalamu kutoka Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Mimea (National Herbarium of Tanzania), amesema kitengo hicho hukusanya sampuli za mimea na kufanya utambuzi wa kisayansi ili kubaini aina zake, hasa mimea isiyofahamika ambayo inaweza kuwa vamizi.

Mollel amesema mimea vamizi inaweza kuenea kwa kasi na kuathiri uzalishaji wa mazao kwa kushindana na mimea ya chakula, hali inayoweza kupunguza mavuno ya wakulima. Pia, mimea hiyo inaweza kuathiri maeneo ya malisho kwa kuenea na kuchukua nafasi ya mimea inayoliwa na mifugo na wanyamapori, hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula cha mifugo.

Amesema utambuzi wa mapema wa mimea vamizi ni muhimu ili kuwezesha hatua za udhibiti kuchukuliwa kabla haijaenea na kusababisha madhara makubwa kwa kilimo na mazingira. Juhudi hizo zina mchango katika kulinda uzalishaji wa chakula na kuimarisha usalama wa chakula nchini.


Naye, Mapulish D. Hebel kutoka Kitengo cha Teknolojia za Vinyunyizi vya Viuatilifu cha TPHPA amesema mamlaka hiyo husimamia usajili na ukaguzi wa vifaa vya kunyunyizia viuatilifu vinavyoingia nchini ili kuhakikisha vinakidhi vigezo vya ubora na vinafaa kwa matumizi ya kilimo.

Hebel amesema mamlaka hiyo pia hutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi na salama ya viuatilifu, namna ya kudhibiti visumbufu vya mimea na mbinu bora za kunyunyizia dawa. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanalenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kupunguza madhara ya viuatilifu kwa afya ya binadamu na mazingira.

Kwa upande wake, Masoud Matimbwa kutoka Kitengo cha Kudhibiti Visumbufu vya Mlipuko cha TPHPA amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kudhibiti kwelea kwelea kwa kiwango kikubwa katika maeneo ya Babati, Moshi, Pwani na Kilosa, hatua inayosaidia kulinda mazao ya wakulima na kuongeza kipato chao.

Matimbwa amewataka wakulima kukagua mashamba yao mara kwa mara na kutoa taarifa mapema wanapobaini dalili za uvamizi wa visumbufu vya mimea ili hatua za udhibiti zichukuliwe kabla havijasababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Amesema utambuzi wa mapema utasaidia kuokoa mazao na kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula.

Akizungumza, Alfred Kiraho, mtaalamu kutoka Idara ya Usimamizi wa Viuatilifu ya TPHPA, amewashauri wafanyabiashara wanaosafirisha mazao nje ya nchi kupeleka sampuli maabara kupima masalia ya viuatilifu kabla ya kusafirisha, na hatua hiyo husaidia kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya usalama vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa, huku majibu ya maabara hiyo yakiaminika na kukubalika duniani.

 

Na.Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussain Bashe, amesema wadau wote wa zao la tumbaku watakaoshindwa kushiriki katika zoezi la usajili wa wakulima hawataruhusiwa kufanya kazi na wakulima, ikiwemo vyama vya ushirika nchini.

Mhe. Bashe ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 8, 2025, mjini Tabora, wakati wa kikao kazi kilicholenga kuboresha huduma ya bima ya mazao na kuhakikisha mkulima analindwa dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji.

Amesema bima kwa wakulima ni jambo la lazima kwa sasa, kwani inalenga kuwalinda wanapokumbwa na changamoto kama ukame, magonjwa au majanga mengine ya asili. Alibainisha kuwa Serikali ina muelekeo mahsusi wa kuhakikisha kila mkulima nchini anakuwa na bima ya mazao, ili kujenga misingi ya kilimo biashara chenye tija.

“Ni lazima tuweke mazingira mazuri kwa wakulima kufanya kilimo biashara. Tunataka kila mkulima wa tumbaku awe amesajiliwa na awe na bima ya mazao yake,” amesema  Mhe. Bashe.

Aidha, ameelekeza kuanzishwa kwa bima ya ushirika itakayosimamiwa na Benki ya Ushirika, ambayo itamlinda mkulima kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi mavuno ya tumbaku.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuwa wakulima wa zao hilo mkoani Tabora wafanyiwe usajili wa mashamba yao na wapate bima ya zao hilo, kwani jukumu la Serikali ni kumlinda mkulima,” ameoneza

Pia, Mhe. Bashe ametoa agizo kwa kampuni za ununuzi wa tumbaku kuhakikisha zimelipa madeni yao kwa wakulima kabla ya Oktoba 30 mwaka huu, vinginevyo hazitaruhusiwa kupewa leseni ya kununua tumbaku katika mkoa wa Tabora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, amemshukuru Waziri Bashe kwa hatua anazochukua kulinda maslahi ya wakulima, huku akisisitiza haja ya kufanya mapitio ya mfumo wa sasa wa bima ya tumbaku kutokana na mapungufu yaliyopo ambayo yamekuwa yakiwaathiri wakulima.

Amesema kuna umuhimu wa kuwepo mkakati wa kitaifa wa kuwalinda wakulima dhidi ya hasara zinazotokana na majanga mbalimbali.

.

 

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,akizungumza kwenye kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

WADAU wa zao la Tumbaku nchini wamekutana jijini Dodoma na kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha wakulima wanapata bima ya zao hilo kupitia vyama vyao vya ushirika, ili kuwalinda dhidi ya majanga na hasara zinazoweza kuathiri uzalishaji.

Kikao hicho maalum kimewaleta pamoja Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Konsotia ya Bima za Kilimo (TAIC), taasisi za kifedha na wakuu wa wilaya za mkoa wa Tabora.

Lengo  la mkutano huo ulikuwa  kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wakulima wa tumbaku, hususan uhakika wa kipato wanapokumbana na majanga ya asili au mazingira yasiyotabirika, pamoja na utoroshaji wa mazao.

Akizungumza kwenye kikao hicho Lleo Septemba 17,2025 jijini Dodoma, Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema kuwa hatua hiyo ni mwanzo wa kuhakikisha kila mkulima wa tumbaku anakuwa na bima ya mazao kabla ya kuanza msimu mpya wa kilimo.

“Usajili wa wakulima wa tumbaku utaanza mara moja na takwimu zao zitakusanywa kwa manufaa ya wakulima wenyewe, taasisi za kifedha na kampuni za bima. Tunataka mfumo wa bima uwe na tija na kulinda kipato cha mkulima,” amesema  Dkt. Ndiege.

Aidha ameongeza kuwa bima kwa wakulima kwa sasa ni jambo la lazima kwa kuwa inawalinda wanapokumbwa na majanga, huku akibainisha kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kila mkulima anakuwa na bima ya mazao.

"Kupitia ushirika, wakulima wataweza kupata huduma ya bima kwa urahisi zaidi, huku taasisi za kifedha na kampuni za bima zikihakikisha mfumo huo unakuwa endelevu."amesema Dkt. Ndiege.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis Mkanachi, amesema kuwa usajili na bima kwa wakulima ni hatua ya kudhibiti mianya ya utoroshaji wa tumbaku na kuhakikisha mkulima anakua na maslahi ya moja kwa moja kupitia chama chake cha ushirika.

Dkt.Mkanachi, amesema kuwa usajili wa wakulima ni hatua muhimu na ya haraka, kwani bila ya zoezi hilo uhalali na utambuzi wa wakulima unabaki kuwa fumbo.

 "Kukamilika kwa usajili huo kutasaidia kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa tumbaku, kwa kuwa mkulima atakayekopeshwa na benki kupitia chama cha ushirika atalazimika kuuza tumbaku yake kupitia chama hicho na si vinginevyo."amesema Dkt.Mkanach

Wadau hao wameeleza kuwa bima ya mazao ni nguzo muhimu katika kulinda ustawi wa wakulima na kuongeza tija ya kilimo, jambo litakalosaidia sekta ya tumbaku kuchangia ipasavyo katika pato la taifa.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,akizungumza kwenye kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Kamishna wa Bima  Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) - Dkt. Baghayo Saqware,akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

 Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis Mkanachi,akichangia mada  wakati wa kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt Gerald Mongella,akichangia mada  wakati wa kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,(hayupo pichani) wakati wa  kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,(hayupo pichani) wakati wa  kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,(hayupo pichani) wakati wa  kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

Wadau mbalimbali wakisikiliza hotuba ya Mrajis na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege,(hayupo pichani) wakati wa  kikao cha wadau wa Tumbaku kwa ajili ya kupitisha utaratibu wa utekelezaji na utoaji wa Bima ya Zao la Tumbaku kwa wakulima kupitia Ushirika kilichofanyika leo Septemba 17,2025 jijini Dodoma.

 



Na Mwandishi wetu- Morogoro

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na faida kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa na, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua warsha kuhusu kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Kilimo  leo tarehe 16 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Mbaraka Mshee - Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro.

Dkt. Yonazi alisema, hatua hiyo ni kutokana na Serikali kuongeza najeti ya Kilimo kwa miaka mitatu mfululizo kutoka bilioni 294 (2022/2023) hadi  trilioni 1.241 (2025/2026) ambapo katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua Programu na Mipango ya kufanikisha malengo hayo ambayo ni pamoja na Programu ya BBT, Agenda 10/30 na Agricultural Transformation Master Plan.

“Ninapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuboresha muundo wa Taasisi za Umma na kuanzisha Idara ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika ngazi zote nchini kwa lengo la kupima utendaji wa Serikali,” alisema Dkt. Yonazi.

Pia aliongeza kwamba, warsha hiyo itakayofanyika kwa siku tano itawezeshwa na  wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)  kwa kushirikiana na Mtaalam Mbobezi kutoka Benki ya Dunia kuhusu dhana mbalimbali zikiwemo muundo wa kitaasisi wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini, Mwongozo Elekezi wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali (M&E Operational Manual).


“Mpango mwingine ni  Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango kazi wa Mwaka wa Wizara na Taasisi (M&E Plan), Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (M&E Strategy) na Moduli ya kupima utendaji wa Wizara na Taasisi husika (M&E Performance Model). Aidha, ni muhimu kupima hali ya utayari wa kila Wizara na Taasisi zake,” alieleza .

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu imekasimiwa jukumu la kuratibu, kufuatilia, kutathmini na kupima utendaji wa serikali nchini hivyo ofisi imeendelea kuratibu shughuli hizo kwa kuandaa na kuwasilisha nyaraka muhimu zitakazowezesha ubora na ufanisi wa kazi za ufuatiliaji na tathmini. 

“Ni muhimu kuvisimamia vitengo vyenu kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ili kazi zetu ziwe na ubora unaotakiwa. Aidha, ni matarajio yangu kuwa nyaraka hizo zitawaongoza kuandaa nyaraka elekezi na tendaji kwa kuzingatia muktadha wa Wizara yenu ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu,” alibainisha.

Aidha, Dkt. Yonazi aliwasihi washiriki wa warsha hiyo  kujadili masuala yote ikiwemo changamoto zinazoweza kusababisha kuwa na utekelezaji usioridhisha katika Wizara mbalimbali na Taasisi zake ikiwemo Wizara ya Kilimo pamoja na kupendekeza namna bora ya kuondokana na changamoto hizo.

MWISHO

 Watendaji Wizara Wizara ya Kilimo watakiwa kuanza mchakato wa ununuzi wa ndege mpya tatu kwa ajili ya vituo vya Kilimo anga vya kanda vilivyopo katika mikoa ya Arusha,Mbeya na Mwanza lengo likiwa ni kudhibiti visumbufu vya mimea.


Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, ametoa maagizo hayo wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege moja ya kudhibiti visumbufu vya mimea iliyonunuliwa na Serikali chini ya Wizara hiyo kwenye Kiwanja kidogo cha ndege Mkoani Dodoma ambayo itatumika katika kituo cha Kanda ya Kati.

“Vituo vyote hivi vinatakiwa viwe vina ndege na ‘drones’ kwa hiyo, mchakato wa kununua ndege tatu nyingine uanze sasa hivi. Ni lazima kama Nchi ijitegemee, dunia ya kubebana haipo. Lazima tuweze kutoa huduma, tumeshaanza kununua ‘drones’ za kufanya ‘survilence’, mwaka huu tunanunua drone kwa ajili ya ‘spraying’.” Mhe. Bashe.

Kadhalika, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru, amesema ndege hiyo inalenga kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa kuleta tija, ajira na kupanua masoko lakini pia kuimarisha hali ya chakula hapa nchini na kuongeza kuwa visumbufu vya mimea ni moja ya jitihada za Mamlaka katika kuleta tija kwenye sekta hiyo.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa ununuzi wa Ndege hiyo ambayo italeta matumaini kwa Mkulima.

“Utashi huu unakwenda kuleta matumaini kwa Mkulima ambaye si mvivu, kwani amelima na kutunza mazao yake halafu mwishoni ndege anakula. Kwa Mkoa wa Dodoma itatuongezea upatikanaji wa chakula na wale wavivu sasa wataanza kulima kwani Dodoma pia tunapata athari ya Nzige maeneo ya Bahi na Kwelea kwelea maeneo ya Chemba, Kondoa na Kongwa.”

Ndege hiyo ‘Thrush 510 P2’ imegharimu TSh.  6,000,000,000 ina uwezo wa kukaa angani kwa zaidi ya saa 4 kutokana na tenki lake kubeba mafuta yenye ujazo wa lita 863, uwezo wa kubeba viuatilifu lita 1,930 uwezo wa kufanya udhibiti kwenye eneo la ekari 2400 kwa mara moja huku ikiwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma  Kanda ya kati.





Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja amekipongeza Chuo Kikuu  cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa namna ambavyo kimekuwa mstari wa mbele katika kuanzisha programu mbalimbali ambazo zinawasaidia wahitimu wake kujiajiri.

Ameyasema hayo wakati wa halfa ya ugawaji wa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao chuoni hapo mkoani Morogoro . Mha. Luhemeja  amesema kizazi cha leo lazima kiweke dhamira ya dhati katika elimu ili kuweza kutengeneza mustakabali wa Taifa.

Mha. Luhemeja ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ugawaji wa zawadi hizo kuelekea kwenye mahafali ya 44 ya chuo hicho yanayotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 17,2026 ambapo wahitimu 3,060 wanatarajia kuhitimu masomo yao.

“Tutoe elimu bora na inayofaa ili kusaidia kizazi kijacho kipata ujuzi na maarifa muhimu ya kustawi katika ulimwengu unaobadilika kila mara na lazima uwe na ndoto, lakini kumbuka ndoto bila lengo ni kazi bure.

“Lazima kuchukua uchambuzi wa kina ndani yako na kuangalia nini kinakusaidia katika kufanikiwa. Mustakabali wa Taifa hili unakutegemea wewe.  Hakuna kisingizio cha kutojaribu. Usiruhusu kushindwa kwako kukufafanulie wewe ulivyo, bali acha kushindwa kwako kukufundishe,” amesema Mha. Luhemeja. 

Aliongeza kuwa SUA ni moja ya vyuo vikuu vinavyoongoza katika ukanda wetu katika kutoa elimu bora, hivyo lazima kiendelee kutathmini jinsi wahitimu wanavyojiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.

“Serikalini tunakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kubuni nafasi za ajira zaidi ya milioni 8 katika miaka mitano ijayo. Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine  kina jukumu muhimu la kulea wahitimu ambao sio watafuta kazi tu bali pia waundaji wa kazi. 

“Niipongeze SUA kwa mipango yake ikiwemo kuhimiza ujasiriamali na kuwapa wanafunzi ujuzi muhimu wa kujiajiri kwani juhudi hizi ni za kupongezwa na muhimu katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana.

Amesisitiza kwa kuwapongeza SUA namna inavyoshiriki katika mapitio ya mitaala yake ambapo amesema kwa kufanya hivyo inaonyesha kujitolea na kuhakikisha kwamba elimu yake inasalia kuwa muhimu na kuwiana na mahitaji ya soko la kazi la leo.

 


Waziri wa  Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina Mpango wa kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Cha Chai kwa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kuweka miundombinu ya umwagiliaji.

Kuhusu Bei ya chai Waziri Bashe amesema itabaki ile ile ya mwaka jana ya Sh 366.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye mkutano Mkuu wa mwaka wa wadau zao la Chai.

Mkutano huo ulihudhuriwa wakulima wa zao la Chai,wakubwa,wadogo na wa kati, wazalishaji, wachakataji, wachanganyaji, wafungashaji, wafanyabiashara wa ndani na nje.

Washiriki wengine ni Wakuu wa Wilaya na Halmashauri zenye wakulima wa Chai nchini (Rungwe, Busokelo, Njombe, Ludewa, Mufindi, Kilolo, Muheza, Korogwe, Lushoto, Muleba, Bukoba na Tarime).

Waziri wa Kilimo,Hussein Bashe amesema Serikali imeweka mikakati ya kuliendeleza zao la Chai ambapo ina mpango wa kuajiri maafisa ugani 200 ambao watashughulika na wakulima wadogo wadogo wa zao hilo.

Waziri Bashe amesema Wizara ya kilimo inazifahamu changamoto zote za zao la Chai hivyo amezungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuona namna bora ya kuajiri maafisa Ugani ambao watashughulikia zao hilo tu.

"Hawa maafisa ugani maalumu 200 watashughulikia wakulima wadogo wadogo wa zao la chai,"amesema Waziri Bashe.

Pia amesema amezielewa na kuzipokea changamoto zote hivyo waombe Mungu Wizara ya Fedha waweze kuwaelewa watakapoomba fedha.

Aidha amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ina Mpango wa kuendeleza Kilimo cha umwagiliaji Cha Chai kwa kuwasaidia wakulima wadogo wadogo kuweka miundombinu ya umwagiliaji.

"Changamoto zote tunazipitia tunataka sekta ya chai izidi kusonga mbele na niwaambie tutaendeleza majadiliano na Mohammed Enterprises kuhusu yale mashamba," amesema Waziri Bashe.


Naye,Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Mweli amesema bado Kuna changamoto za uzalishaji na bei ambapo Wizara inaendelea kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania Mary Kipeja amesema wana Mpango wa kujenga viwanda vitano vya Chai nchini.

Pia amesema wana Mpango wa kujenga mifumo ya umwagiliaji na wataanza Wilayani Njombe.

Kipeja amesema Mkutano huo hufanyika mara moja kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wadau wote wa ndani na nje ya Tanzania kwa ajili ya kujadiliana kuhusu mafanikio, changamoto na fursa ili kubuni, kujadili na kuweka mikakati ya kuendeleza tasnia ya chai. 

Amesema katika mkutano wa jukwaa la wadau wa mwaka 2024, mada Kuu zitakazojadiliwa ni pamoja na,Kupitia muhtasari na taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa wadau wa zao la Chai uliofanyika Januari 18, 2023 Mkoani Iringa.

Pia,Kuwasilisha taarifa ya mwenendo wa Tasnia ya Chai nchini ikiwa ni Pamoja na usajili wakulima wa zao la Chai,Uhamasishaji maendeleo ya Tasnia ya Chai.

Vilevile Uendelezaji wa zao la Chai katika Wilaya ya Kilolo Mkoani Iringa,Maendeleo ya mnada wa Chai wa kimtandao Dar Es Salaam, Hali ya ulipaji wa madeni sugu ya wakulima wa Chai nchini.

Pia,Hali ya uendeshaji wa viwanda vya uchakataji wa chai,Upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za Chai (Miche bora, mbolea na viuagugu).

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa kamati ya Kilimo,Viwanda na Mifugo,Deo Mwanyika amesema iko haja ya kuangalia wawekezaji wengine kutokana na baadhi ya waliopo kutokufanya vizuri.


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na usimamizi wa fedha ujenzi wa miradi ya Umwagiliaji katika mashamba ya Taasisi ya Utafiti wa Mbegu (TARI) pamoja na Mashamba ya Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) ikiwemo shamba la mbegu Ngaramtoni pamoja na shamba la mbogamboga Tengeru mkoani Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Daniel Sillo (Mb) amesema wajumbe wa Kamati hiyo wameridhishwa na miradi waliyo tembelea ambapo wamesema kuwa miradi hiyo ilitengewa fedha na serikali na kamati hiyo ndio iliyosimamia utengaji wa fedha hizo hivyo kuna kila sababu ya kamati kukagua nakuona thamani ya fedha ilivyotumika katika sekta ya Umwagiliaji.

Amesema miradi hiyo kwa Shamba la Arusha yenye thamani ya Billion 4.4 ikikamilika itaongeza upatikanaji wa Mbegu bora za kilimo Kwa wananchi na kupunguza uaigizaji wa Mbegu kutoka Nchi za nje.

Mwenyekiti Sillo amesema katika sekta ya kilimo Kamati hiyo inamatumaini makubwa ya kupata matokeo chanya ya ukamilishaji wa miradi nakuona matokeo chanya katika Mirada hiyo.

Amesema mpaka sasa Kamati hiyo haina mashaka ya matumizi ya fedha za umma kutokana na kuonekana kwa thamani ya fedha ilivyo tumika.

Aidha ameipongeza Kampuni inayojenga miundombinu hiyo ya Umwagiliaji Pro Agro Global ltd kwa kufanya kazi Kwa uzalendo na kuonesha kuwa vijana wakipewa kazi wanaweza.