Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mha. Cyprian Luhemeja amekipongeza Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa namna ambavyo kimekuwa mstari wa mbele katika kuanzisha programu mbalimbali ambazo zinawasaidia wahitimu wake kujiajiri.
Ameyasema hayo wakati wa halfa ya ugawaji wa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao chuoni hapo mkoani Morogoro . Mha. Luhemeja amesema kizazi cha leo lazima kiweke dhamira ya dhati katika elimu ili kuweza kutengeneza mustakabali wa Taifa.
Mha. Luhemeja ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ugawaji wa zawadi hizo kuelekea kwenye mahafali ya 44 ya chuo hicho yanayotarajiwa kufanyika kesho Oktoba 17,2026 ambapo wahitimu 3,060 wanatarajia kuhitimu masomo yao.
“Tutoe elimu bora na inayofaa ili kusaidia kizazi kijacho kipata ujuzi na maarifa muhimu ya kustawi katika ulimwengu unaobadilika kila mara na lazima uwe na ndoto, lakini kumbuka ndoto bila lengo ni kazi bure.
“Lazima kuchukua uchambuzi wa kina ndani yako na kuangalia nini kinakusaidia katika kufanikiwa. Mustakabali wa Taifa hili unakutegemea wewe. Hakuna kisingizio cha kutojaribu. Usiruhusu kushindwa kwako kukufafanulie wewe ulivyo, bali acha kushindwa kwako kukufundishe,” amesema Mha. Luhemeja.
Aliongeza kuwa SUA ni moja ya vyuo vikuu vinavyoongoza katika ukanda wetu katika kutoa elimu bora, hivyo lazima kiendelee kutathmini jinsi wahitimu wanavyojiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo.
“Serikalini tunakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kubuni nafasi za ajira zaidi ya milioni 8 katika miaka mitano ijayo. Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine kina jukumu muhimu la kulea wahitimu ambao sio watafuta kazi tu bali pia waundaji wa kazi.
“Niipongeze SUA kwa mipango yake ikiwemo kuhimiza ujasiriamali na kuwapa wanafunzi ujuzi muhimu wa kujiajiri kwani juhudi hizi ni za kupongezwa na muhimu katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira kwa vijana.
Amesisitiza kwa kuwapongeza SUA namna inavyoshiriki katika mapitio ya mitaala yake ambapo amesema kwa kufanya hivyo inaonyesha kujitolea na kuhakikisha kwamba elimu yake inasalia kuwa muhimu na kuwiana na mahitaji ya soko la kazi la leo.
Post A Comment: