Na.Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussain Bashe, amesema wadau wote wa zao la tumbaku watakaoshindwa kushiriki katika zoezi la usajili wa wakulima hawataruhusiwa kufanya kazi na wakulima, ikiwemo vyama vya ushirika nchini.

Mhe. Bashe ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 8, 2025, mjini Tabora, wakati wa kikao kazi kilicholenga kuboresha huduma ya bima ya mazao na kuhakikisha mkulima analindwa dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji.

Amesema bima kwa wakulima ni jambo la lazima kwa sasa, kwani inalenga kuwalinda wanapokumbwa na changamoto kama ukame, magonjwa au majanga mengine ya asili. Alibainisha kuwa Serikali ina muelekeo mahsusi wa kuhakikisha kila mkulima nchini anakuwa na bima ya mazao, ili kujenga misingi ya kilimo biashara chenye tija.

“Ni lazima tuweke mazingira mazuri kwa wakulima kufanya kilimo biashara. Tunataka kila mkulima wa tumbaku awe amesajiliwa na awe na bima ya mazao yake,” amesema  Mhe. Bashe.

Aidha, ameelekeza kuanzishwa kwa bima ya ushirika itakayosimamiwa na Benki ya Ushirika, ambayo itamlinda mkulima kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi mavuno ya tumbaku.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuwa wakulima wa zao hilo mkoani Tabora wafanyiwe usajili wa mashamba yao na wapate bima ya zao hilo, kwani jukumu la Serikali ni kumlinda mkulima,” ameoneza

Pia, Mhe. Bashe ametoa agizo kwa kampuni za ununuzi wa tumbaku kuhakikisha zimelipa madeni yao kwa wakulima kabla ya Oktoba 30 mwaka huu, vinginevyo hazitaruhusiwa kupewa leseni ya kununua tumbaku katika mkoa wa Tabora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, amemshukuru Waziri Bashe kwa hatua anazochukua kulinda maslahi ya wakulima, huku akisisitiza haja ya kufanya mapitio ya mfumo wa sasa wa bima ya tumbaku kutokana na mapungufu yaliyopo ambayo yamekuwa yakiwaathiri wakulima.

Amesema kuna umuhimu wa kuwepo mkakati wa kitaifa wa kuwalinda wakulima dhidi ya hasara zinazotokana na majanga mbalimbali.

.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: