Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Chunya Mhandisi Laurent Mayala amesema ongezeko la shughuli za madini Chunya zimeleta mageuzi makubwa  na hivyo  kuchochea ukuaji wa sekta nyingine ikiwemo uzalishaji wa madini ya dhahabu ambapo hivi sasa umefikia  kilo 300 kwa mwezi kutoka kilo 5 mwaka 2017/18.

Amesema kwamba, mwenendo  wa biashara ya madini Chunya unakwenda vizuri huku shughuli nyingine zinazotazamiwa kukamilika  na zilizoko mbioni kuanza zinatarajia  kuifanya Chunya kuwa kioo  kwa sekta ya madini  nchini na kuuelezea mwenendo wa biashara  ya dhahabu pekee kwamba unaendelea kuacha alama ya ukuaji wa mji huo huku ikichochea shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii.

‘’Mwenendo wa mauzo ya dhahabu kwa mwaka 2023/24 zilizalishwa dhahabu zenye uzito wa tani 3.1 za thamani ya shilingi bilioni 452.2 huku tozo, mrabaha na ada za ukaguzi za Serikali zilikusanywa shilingi bilioni 31, mwaka 2024/25 zilizalishwa dhahabu zenye uzito wa tani 3.9 za thamani ya shilingi bilioni 820.9 na tozo za serikali  zilikuwa shilingi bilioni 55,’’ amesema  Mhandisi Mayala.

Ameongeza ongezeko  la uzalishaji wa dhahabu  limechochewa na uwepo wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi ambapo  hivi sasa kuna vituo vidogo vya ununuzi wa dhahabu vipatavyo 24 na soko  kuu moja lililojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa lengo la kurahisisha biashara ya madini wilayani humo.  Chunya ilikuwa mkoa wa pili wa kimadini kuanzisha soko la madini mwezi Mei 2019, lililotanguliwa na soko kuu la Geita lililoanzishwa mwezi Machi, 2019. Mkoa wa kimadini Chunya unatajwa kuwa wa pili kwa uzalishaji wa dhahabu nchini ukitanguliwa na Geita.

‘’ Hadi sasa katika robo ya kwanza ya mwaka 2025/26 tayari tumekwisha kusanya shilingi bilioni 19.13 sawa na asilimia 26.5, Lengo ni kukusanya shilingi bilioni 72, nina imani tutafikia lengo la ukusanyaji tulilopangiwa,’’ amesema Mhandisi Mayalla.

Akizungumzia historia ya mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli  mkoani humo, amesema  mwaka 2023/24 mkoa huo ulikusanya shilingi bilioni 37.3 sawa na asilimia 84.7  ya lengo la  shilingi bilioni  44 ilizopangiwa kukusanya; mwaka wa fedha  2024/25 zilikusanywa shilingi bilioni  55.37  sawa na asilimia 92 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 60.2.

 Mradi wa Uzalishaji wa Madini ya Shaba Waanza Kuzaa Matunda

Akizungumzia mchango wa madini mengine, amesema uwepo wa  kiwanda cha kuchenjua  shaba kilichoanzishwa mwezi Aprili 2025 na kinachomilikiwa na Kampuni ya Mineral Acess Limited (MAST)  kilichopo eneo la  Mbugani Chunya hadi sasa tayari kimezalisha tani 810 za shaba zenye thamani ya shilingi bilioni10.3 na tayari kiasi cha shilingi milioni 594 kimekwisha kulipwa Serikalini.

Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu Chaanza Majaribio, Kuiuzia dhahabu BoT na Nje

 Mhandisi Mayala amesema  tayari kiwanda cha Kusafisha madini ya dhahabu kinachomilikiwa na kampuni ya Giant Machine's and Equipments Limited kimekwisha fanya majaribio ya kusafisha dhahabu  ya kilo 2.9 kwa kiwango cha kuuzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania  na nje ya nchi na kwamba, kiwanda hicho kitasafisha dhahabu  zitakazozalishwa wilayani humo na zile za kutoka maeneo mengine.

Maabara ya GST Yasubiriwa na Wadau

 Katika kuwahakikishia wachimbaji wanafanya shughuli zao kwa uhakika na tija, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania iko katika hatua za awali za ujenzi wa maabara ya kisasa ya upimaji sampuli za madini  wilayani Chunya, kama ambavyo tayari imefanyika kwa  Mkoa wa Geita na Dodoma ambapo ujenzi unaendelea. Akizungumzia uwepo wa maabara hiyo, Mhandisi Mayala amesema wachimbaji wanasubri kwa hamu kubwa kukamilishwa kwa maabara hiyo na kueleza kwamba italeta manufaa makubwa Chunya.

 Bado kuna Fursa  za  Kuwekza  Chunya Sekta ya Madini

Aidha, Mhandisi Mayala ametoa wito kwa wananchi na wadau kutoka ndani na nje ya nchi kwamba bado kuna fursa nyingi za kuwekeza chunya kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji madini, uchenjuaji, biashara ya madini, kutoa huduma migodini na ujenzi wa CIP  na nyingine.

Naye Mwenyekiti wa Soko la Madini Chunya ambaye ni mchimbaji, muuzaji na mnunuzi wa dhahabu  Kenneth Mwakyusa  amesema uwepo wa masoko na vituo vya ununuzi vimeleta nafuu kubwa kwa wachimbaji, wauzaji na wanunuzi wa dhahabu kutokana na uwepo wa bei elekezi, kupanda thamani ya dhahabu na kuongeza kwamba, uwepo wa masoko umeleta ajira , yamerahisisha kazi na  maendeleo  kwa Wilaya ya chunya.

‘’ Thamani ya dhahabu imepanda sana, hivi sasa gramu moja kufikia hadi shilingi laki tatu (300,000/=),  Serikali imetusaidia sana, dhahabu imeibadili sana Chunya, Chunya ya mwaka 2015 si sawa na sasa kuna tofauti kubwa sana. Niwaombe wachimbaji na wafanyabiashara tuyatumie masoko ya madini badala yakufanya biashara nje ya masoko,’’ amesema Kenneth

Ombi kwa Serikali

Mwakyusa ameiomba Serikali kuona namna ya kusaidia kupunguza gharama kwenye vifaa vya uchimbaji ili vipatikane kwa bei nafuu. Pia, ameiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza kodi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka asilimia 2 na kubaki asilimia 1.


 Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

Share To:

Post A Comment: