Kuelekea kwenye Zoezi la uchaguzi Mkuu wa Tanzania Jumatano ya Oktoba 29, 2025, Viongozi wa dini, kijamii pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dodoma wameungana pamoja kuhimiza amani, wakiitaja kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Kijamii, kiuchumi, Viongozi wa dini wakisema amani ndiyo Neema muhimu zaidi kwenye nchi yoyote duniani.
Mchungaji Pendo Yohana kutoka Kijiji cha Michese, Askofu Antony Saimon, Mwenyekiti wa Umoja wa madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma pamoja na Sheikh Ahmed Said Ahmed, Msemaji wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, ni miongoni mwa Viongozi wa dini wanaohamasisha kuhusu amani, wakisisitiza kila Mtanzania kuwa Mlinzi wa amani na kujiepusha na matendo yote yenye kuhatarisha amani iliyopo.
Kulingana na tafiti mbalimbali zinaonesha uwepo wa uhusiano kati ya amani na maendeleo katika ujenzi wa Taifa bora na lenye uchumi imara pamoja na kuruhusu kupatikana kwa mahitaji muhimu ya binadamu na huduma stahiki ikiwemo elimu bora, afua bora na ulinzi na usalama kwa wote.
Aidha kwa Upande wake Emmanuel Kamome, dereva wa Bodaboda Mkoani Dodoma pamoja na Shukuru Chimwaga, Msemaji wa Chama cha waigizaji Mkoa wa Dodoma wametoa wito pia wa kulinda amani iliyopo nchini, wakiahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha ulinzi wa amani hasa wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wananchi hao wa Dodoma wameungana na Viongozi na wagombea mbalimbali wa nafasi za Urais wa Tanzania akiwemo Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pamoja na wengine wamekuwa wakitahadharisha Vijana na Jamii kutokubali kutumika na wasioitakia mema Tanzania na kuweza kuvuruga na kuhatarisha amani ya Tanzania kwa kisingizio cha uchaguzi Mkuu, wakisisitiza kuwa uchaguzi ni tendo la kidemokrasia na sio sababu ya machafuko na vurugu kwenye Jamii.
Post A Comment: