Na John Walter-Manyara

Baada ya miaka 13 kupita tangu mkoa wa Manyara upate Fursa ya kuwasha Mwenge wa Uhuru mwaka 2010, na sasa ni bahati nyingine tena ya kuuzima Mwenge huo mwaka 2023 baada ya kumulika halmashauri 195 za mikoa yote 31 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kilele cha Mwenge wa uhuru kinakwenda Sambamba na misa takatifu kwa ajili kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa hili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba 14  itakayoongozwa na Baba Akofu Antony Lgwen wa Jimbo Katoliki la Mbulu ikitanguliwa na wiki ya Vijana.

Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo kubwa ya Kitaifa itakayofanyika katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan.

Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Manyara utakagua na kuweka mawe ya msingi pamoja na kuzindua miradi ya Maji, Afya,Elimu na Miundombinu ya bara bara.

Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 mkoani Manyara Samwel Pastori anasema maandalizi yanaendelea vizuri kwenye maeneo yote huku akiwahimiza wenye nyumba za kulala wageni kuboresha zaidi na hata wanaoendelea kujenga kukamilisha ili watakaofika wapate pa kufikia.

Amesema uwanja wa Kwaraa ambao utatumika upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Aidha amewasisitiza wafanyabiashara wa chakula kuzingatia usafi, wanaojishugulisha na huduma za usafiri kuwa waaminifu ili wageni watakofika wakasimulie huduma nzuri watakayopatiwa. 

Ameeleza kuwa wageni watakaowasili mkoani hapa watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vilivyopo kama hifadhi za Taifa za Tarangire, Ziwa Manyara, Mlima Hanang na mji wa Madini ya Tanzanite (TANZANITE CITY).

Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema "Tunza Mazingira,Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe hai na uchumi wa Taifa".

Kote huko Mwenge ulipopita chini ya Kiongozi Abdalla Shaib Kaim, umefanya kazi ya kuhamasisha amani, Umoja, Upendo na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuwahimiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao pamoja na kuacha matumizi ya dawa za kulevya.

 

Share To:

Post A Comment: