
Baraza la Ushindani (FCT) limeendesha mafunzo ya uwezeshaji kwa wadau mbalimbali jijini Moshi, mkoani Kilimanjaro,katika ukumbi wa Kiringe. Mafunzo hayo yaliwahusisha wafanyabiashara na wananchi kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu masuala ya ushindani, haki za kibiashara na mifumo ya kisasa ya utoaji wa haki.
Mafunzo hayo yalijibiwa kwa mwitikio mkubwa, ishara kuwa kuna mahitaji makubwa ya elimu kuhusu taratibu za kisheria na huduma zinazotolewa na Baraza la Ushindani.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Msajili wa Baraza, Mhe. Mbegu Kaskasi, amewashukuru wadau wa Moshi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha hamasa ya kujifunza, akisema hatua hiyo inaonyesha utayari wa jamii kuimarisha mazingira ya biashara yenye ushindani wa haki.
Mhe. Kaskasi amebainisha kuwa Baraza linaendelea kuboresha mifumo yake ili kurahisisha upatikanaji wa haki, ikiwemo mfumo wa kielektroniki wa uwasilishaji wa mashauri ya rufaa (e-filing), ambao umepunguza gharama na kuondoa usumbufu wa kusafiri kwa wale waliokuwa wakilazimika kufika ofisini moja kwa moja.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kunufaika na elimu waliyoipata, wakisema imewasaidia kuelewa haki zao, wajibu wao na hatua za kufuata wanapohitaji kuwasilisha mashauri yao.


Post A Comment: