Na OWM - TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, leo amepokea mpango mkakati wa ukamilishaji wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa (Mshitiri), Msanifu Majengo Justine Katabalo wa Kampuni ya MCB Company Ltd (Mkandarasi) pamoja na Mhandisi Khamadu Kitunzi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (Mshauri Elekezi), ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa Januari 17, 2026 mjini Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo.
Prof, shemdoe ameridhishwa na mpango mkakati uliowasilishwa ambao utawezesha jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kukamilia ifikapo Juni 07, 2026 tofauti na maelekezo ya awali ambapo ilipaswa jengo hilo kukamilika mwezi Julai 2026.
Awali, Prof. Shemdoe alielekeza ndani ya wiki moja Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mkandarasi kampuni ya MCB Company LTD na Mshauri Elekezi Wakala wa Majengo (TBA) kukutana na kuandaa mpango mkakati wa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kuuwasilisha ofisini kwake leo.
Prof. Shemdoe alilazimika kutoa maelekezo hayo baada ya kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, licha ya kutokuwa na changamoto ya fedha. Ujenzi wa jengo hilo ulianza kutekelezwa Mei 27, 2022 na ulitakiwa kukamilika Mei 26, 2024.










Post A Comment: