Na OWM -TAMISEMI 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM- TAMISEMI) Mhe. Sospeter Mtwale amewataka watendaji wa Sekretarieti za Mikoa kutafakari na kutathmini maeneo ya utendaji kazi yanayohitaji kufanyiwa maboresho pamoja na kujenga timu za utendaji kazi zenye kuleta tija.

Mhe. Mtwale ametoa rai hiyo leo Januari 26, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa St Gasper Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa makatibu tawala wa mikoa sehemu ya elimu na mafunzo ya ufundi, wakuu wa vitengo vya uhasibu na fedha, ukaguzi wa ndani na maendeleo ya jamii kutoka katika sekretarieti za mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Amesema TAMISEMI imeona umuhimu wa kutoa mafunzo ya uongozi kwa watendaji hao ili kuongeza ufanisi na tija katika sekretarieti za mikoa na kuwa awamu hii inahitimisha mafunzo kwa watendaji wa sekretarieti hizo ambapo tayari mafunzo yameshatolewa kwa wakuu na sehemu na vitengo vingine.

"Sitarajii ushiriki hafifu, matarajio ya TAMISEMI baada ya mafunzo ni kuwa mtaweza kusimamia watumishi pamoja na ninyi wenyewe kuwa vioo katika kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na pia mtadhibiti uvujaji wa siri za serikali, mtasimamia vema rasilimali za umma na kuepuka migogoro isiyo ya lazima," amesisitiza Mhe. Mtwale.

Mkurugenzi wa Idara ya Serikali za Mitaa, OWM-TAMISEMI Angelista Kihaga amesema mafunzo hayo ni ya uongozi sio ya taaluma na kuongeza kuwa baada ya mafunzo hayo watafanya tathmini kuona endapo kuna mabadiliko.

Bi. Angelista amewataka watendaji hao wanaopata mafunzo kuwa chachu ya mabadiliko ya uongozi kwa watendaji na watumishi wenzao kwani baadhi ya mada watakazofundishwa ni pamoja na usimamizi wa miradi, rasilimali watu na kufanya kazi kama timu moja.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa, OWM-TAMISEMI Beatrice Kimoleta amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa mwezi Mei 2025 kwa baadhi ya viongozi wa sekretarieti za mikoa kwa kushirikiana vizuri na Taasisi ya Uongozi.

Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo wamelenga kuwajengea uwezo watendaji hao ili wawe washauri wazuri kwa viongozi wa sekretarieti za mikoa kwani hapo awali mafunzo ya uongozi yalikuwa yakitolewa kwa viongozi pekee na kutowashirikisha washauri wao.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Emmanueli Tesua ameishukuru OWM-TAMISEMI kwa kuwashirikisha katika kutoa mafunzo hayo kwa viongozi wote wa Sekretarieti za Mikoa.

Share To:

Post A Comment: