Na Elizabeth Joseph, Monduli.


SERIKALI kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeahidi kuendeleza ustawi wa mahusiano mazuri baina ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi na jamii inayozunguka maeneo hayo.

Kauli hiyo imetolewa wilayani Monduli na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mh, Innocent Bashungwa wakati akiongea na Viongozi wa Mila(Laigwanani) katika kikao maalum kilichoandaliwa na Mbunge wa Monduli Fedrick Lowassa chenye lengo la kujadili mahusiano ya wananchi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi.

Mh,Bashungwa alibainisha kuwa kumekuwa na mahusiano mazuri baina ya Jeshi na wananchi wanaozunguka maeneo yenye kambi za jeshi na kuongeza kuwa ni muhimu kuendeleza misingi ya mashirikiano baina ya pande zote mbili ili kuleta umoja na amani.

"Nimefurahi hakuna mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji na Jeshi ila ipo ya mtu binafsi tu ambayo nawaomba muendelee kuwa na subra sababu jambo hili lipo mahakamani hivyo tusubiri Mahakama ifanye kazi yake"alifafanua Waziri Bashungwa.

Aidha aliwaomba Wazee hao kuendelea kumpa Ushirikiano Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutimiza majukumu ikiwa ni pamoja na kumuombea ili atimize malengo mazuri aliyolenga kuwafanyia watanzania.

Awali Mbunge wa Jimbo la Monduli Mh,Fredrick Lowassa alipongeza Wilaya ya Monduli kuwa sehemu ya mafunzo ya kijeshi na kuomba busara itumike kutatua changamoto zinazojitokeza baina ya Jeshi na wananchi hasa katika eneo la malisho ya mifugo ili kuepusha matumizi ya silaha yanayoweza kuondoa uhai wa binadamu.

"Ombi letu shida inapotokea sababu ya malisho ya mifugo yetu silaha ya Jeshi isitumike kuua kwakuwa kazi ya Jeshi ni kulinda mipaka ya nchi sio kuua wanabchi,basi mahusiano mazuri yaliyokuwepo awali yaendelezwe"aliongeza kusema Mbunge huyo.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Wazee hao Olei Nginei aliomba serikali kupitia Wizara hiyo kuweka maandishi yatakayoonesha wazi maeneo ya mafunzo ya kijeshi na malisho katika vibao vinavyoonesha maeneo hao ili kuzuia shughuli nyingine kufanyika katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa makazi.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mh,Joshua Nassari aliwaomba viongozi hao kuhakikisha wanatumia mifugo yao vizuri kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa kuwapeleka watoto wao Shule ili elimu iweze kuwasaidia katika maisha yao yajayo.

"Tuzingatie umuhimu wa elimu,Mkoa wetu umetoa Mawaziri wakubwa sana wawili ambao ni Hayati Sokoine na Mheshimiwa Edward Lowassa na wao walitoka kwenye jamii ya kifugaji na kwa kutambua umuhimu wa elimu walisoma hata kufikia nyadhifa walizopata hivyo nasie hatuna budi kutambua umuhimu wa kupeleka watoto shule ili wapate elimu"aliongeza kusema Mh, Nassari.

Share To:

Post A Comment: