Mbunge wa Jimbo la Lushoto Prof. Riziki Shemdoe ameishukuru Taasisi ya The Sunshine Muslims Volunteers (SMV) yenye makazi yake jijini Dar es Salaam kwa kufadhili matibabu ya macho kwa wananchi 811 wa Lushoto, mkoani Tanga, yaliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kuanzia tarehe 29 hadi 31 Disemba, 2025.
Miongoni mwa wananchi hao 811 wa Jimbo la Lushoto waliopatiwa huduma ya uchuguzi wa macho, 104 walifanyiwa upasuaji wa macho, 312 walipatiwa miwani ya macho na 267 walipatiwa miwani ya kujikinga na mionzi ya jua.
Kutokana na huduma hiyo, Prof. Shemdoe ameishukuru taasisi hiyo leo Januari 01, 2026 jimboni Lushoto, wakati akizungumza na Mweka Hazina wa taasisi hiyo Dkt. Juma Mzimbiri ambaye ni Daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili MOI.
Aidha, Mhe. Prof. Shemdoe ametoa shukrani zake za dhati kwa Daktari Bingwa wa macho na timu yake kwa kuendesha kambi hiyo ya matibabu kwa kushirikiana wa Mganga Mkuu wa Wilaya pamoja na madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Lushoto.
Akizungumzia diplomasia ya mashirikiano, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutengeneza diplomasia ya mashirikiano na nchi mbalimbali, ambayo imewezesha wananchi wa majimbo ya Lushoto, Mlalo na Bumbuli kunufaika na huduma hiyo.
“Ninawaomba wadau hawa waendelee kutoa udhamini huu wa huduma ya matibabu ya macho, natamani uwe endelevu kila mwaka ili wananchi wengi zaidi wanufaike,” amesema Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, ana imani kuwa wadau hao wataendelea kuona umuhimu wa kusaidia watu, kama ambavyo kauli mbiu yao inavyosema kuwa We Serve to Please Allah yaani wanasaidia ili kupata radhi ya Mwenyezi Mungu.
Naye, Mweka Hazina wa SMV Dkt. Juma Mzimbiri amesema kuwa, kambi ya matibabu imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi ambao wamejitokeza kwani wamepatiwa huduma ya uchuguzi wa macho, upasuaji wa macho, na kupatiwa miwani za macho pamoja na za kujikinga na mionzi ya jua.
Kuhusiana na jitihada za kutafuta wadau wengine, Dkt. Mzimbiri kumshukuru Prof. Shemdoe kwa kuendelea kushirikiana na taasisi yake ya SMV katika kutafuta wadau ambapo mdau YERYUZ DOKTORLARI alipatikana na kushiriki kutoa huduma katika kambi ya matibabu.

Post A Comment: