Na Mwandishi Maalumu – Arusha

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema taasisi hiyo imejipanga kuimarisha huduma za matibabu ya moyo katika Kanda ya Kaskazini pamoja na huduma nyingine zinazotolewa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwa lengo la kuifanya hospitali hiyo kuwa kituo cha mfano barani Afrika katika utoaji wa huduma za moyo.

Dkt. Kisenge ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wazabuni wa dawa za binadamu, vifaa tiba na vitendanishi katika kikao kilichofanyika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambapo alisema mafanikio ya taasisi yoyote ya tiba yanategemea uwajibikaji wa pamoja wa wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa utoaji huduma.

Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishiba ya damu ya moyo iliyoziba aliwaomba wazabuni hao kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na kwa wakati huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya kufanikisha utendaji wa ALMC.

“Kwa sasa JKCI inaisimamia ALMC na tayari imeanza kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ya huduma na mifumo ya kazi ili kuhakikisha huduma za moyo na magonjwa mengine zinatolewa kwa viwango vya juu vya kitaalamu, mafanikio ya hospitali hii yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa pamoja kati ya wafanyakazi, wazabuni na wadau wote wa sekta ya afya”, alisema Dkt. Kisenge.

Akizungumzia hatua za baadaye Dkt. Kisenge alisema ALMC itaanza kutoa huduma za kibingwa zaidi ikiwemo uwepo wa maabara ya uchunguzi na matibabu ya  mishipa ya moyo (Cath Lab) pamoja na upasuaji wa kufungua kifua hatua itakayopunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya mkoa na nchi sambamba na kuimarisha dhana ya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa matibabu barani Afrika.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bunare Daniel alisema watashirikiana na wazabuni hao ili upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na vitendanishi unakuwa wa haraka na wa uhakika. Kila hatua watakayoichukuwa italenga kuondoa ucheleweshaji katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

“Ushirikiano wetu na nyinyi ni muhimu sana ili wagonjwa wapate matibabu ya haraka, salama na ya ubora wa juuTunafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bila kuchelewa au kukosa vifaa muhimu”,

“Tunawahimiza wadau wote kushirikiana nasi kwa karibu ili huduma za moyo na magonjwa mengine ziwe bora zaidihuku tukihakikisha kila hatua katika upatikanaji wa vifaa inafanyika kwa uwazi, haraka na kwa ufanisi”, alisema Bunare.

Kwa upande wao  wazabuni hao waliushukuru uongozi wa JKCI kwa kuitisha kikao hicho huku wakisema kimewapa fursa ya kubadilishana mawazo, kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha ushirikiano wao na taasisi hiyo katika kuboresha huduma za matibabu.

Meneja wa Maendeleo ya Biashara kutoka Pacific Diagnostics, Salmaan Karim alisema JKCI ni miongoni mwa taasisi chache wanazofanya nazo kazi kwa urahisi na ushirikiano mzuri ikilinganishwaa taasisi nyingine.

Meneja Msaidizi wa Mauzo kutoka Cardimed Africa L.t.d, Linda Tegambwage alisema kikao hicho kimeimarisha uelewa na mahusiano kati ya wazabuni na uongozi wa JKCI, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wazi na mawasiliano ya mara kwa mara ni msingi wa kuhakikisha vifaa tiba na huduma zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaokidhi mahitaji ya wagonjwa.

Share To:

Post A Comment: