Mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi Afrika Mashariki (EACOP) unaendelea kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa wananchi wa Tanzania na Uganda, huku ukiendelea kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.
Hayo yameelezwa wakati wa ziara rasmi ya Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, aliyeko nchini kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga. Waziri huyo yuko nchini sambamba na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Ndejembi amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa EACOP umeendelea kuleta manufaa makubwa, hususan katika eneo la ajira, ambapo jumla ya ajira 12,000 zimetolewa kwa vijana na wananchi wa Tanzania na Uganda tangu kuanza kwa mradi huo.
Ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki umefikia asilimia 79 ya utekelezaji, na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai 2026. Aliongeza kuwa mradi huo utaongeza mapato ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi, sambamba na kuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku pindi utakapokamilika.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira na ushirikiano mkubwa unaooneshwa katika utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Dkt. Nankabirwa amesema mradi wa EACOP umeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa nchi za Tanzania na Uganda, na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa utaratibu wa kuwatambua watumishi na wataalamu wanaoshiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati ili waweze kupewa kipaumbele katika miradi mingine ijayo kulingana na uzoefu na uadilifu wao. Ameitaja miradi ya gesi na umeme inayotarajiwa kutekelezwa na nchi hizo mbili kuwa miongoni mwa miradi itakayonufaika na uzoefu huo.
Mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga una urefu wa kilomita 1,443, ambapo kilomita 296 zipo nchini Uganda na kilomita 1,147 zipo nchini Tanzania. Kwa upande wa Tanzania kutakuwa na jumla ya vituo vinne vya kusukuma mafuta, huku Uganda ikiwa na vituo viwili, na kufanya jumla ya vituo vya kusukuma mafuta kuwa sita.


Post A Comment: