Imeelezwa kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kupitia mradi wa EASTRIP ili kukifanya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), kupitia Kituo cha Umahiri Kikuletwa, kuwa kitovu cha mafunzo ya nishati jadidifu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. 

Akizungumza Januari 6, 2026 wakati wa ziara yake katika kituo hicho, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir alisema kuwa utekelezaji wa mradi wa EASTRIP utakifanya ATC kuwa kitovu cha mafunzo ya vitendo katika uzalishaji wa nishati safi ikiwemo nguvu ya maji, jua, upepo na bioanuwai. 

Alielekeza kuwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme utasaidia kutoa wahitimu wenye ujuzi unaohitajika, na kusisitiza umuhimu wa kuwahusisha wakufunzi na wanafunzi moja kwa moja katika ujenzi huo ili kuongeza uwezo wa kitaaluma na kuboresha mafunzo.

Aidha, Naibu Waziri alielekeza chuo kuendelea na kuimarisha mahusiano na viwanda pamoja na taasisi za elimu, sayansi na teknolojia ndani na nje ya nchi. Hatua hiyo inalenga kutoa fursa kwa watumishi na wanafunzi kushiriki katika tafiti za pamoja zinazoweza kujibu changamoto za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Prof. Musa Chacha, alisema kuwa utekelezaji wa mradi wa EASTRIP umewezesha ujenzi wa kituo cha kufua umeme, umeongeza udahili wa wanafunzi hasa wa kike, na kuanzishwa kwa mitaala mipya 27. Pia umewezesha ujenzi wa miundombinu mipya katika Kampasi ya Kikuletwa pamoja na mitambo ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia.

Prof. Chacha aliongeza kuwa ili kuhakikisha utekelezaji wa elimu amali unafanikiwa, chuo kimeweka mkakati wa kuhamasisha wanafunzi kupenda na kuchagua elimu amali hususan katika mafunzo ya nishati jadidifu.








Share To:

Post A Comment: