Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, Mhe. Timontheo Mnzava, amewataka madiwani na wenyeviti wa vijiji kushirikiana kwa karibu katika kutatua migogoro ya ardhi ili kulifanya jimbo hilo kuwa mfano wa matumizi sahihi ya ardhi na kuimarisha amani kwa wananchi.
Mbunge Mnzava ametoa wito huo wakati akiendelea na ziara zake za kukutana na makundi mbalimbali ya jamii, kwa kushirikiana na viongozi wa Chama pamoja na Halmashauri. Katika kikao maalum alichokaa na madiwani pamoja na wenyeviti wa vijiji, walijadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha utawala bora na maendeleo ya wananchi.
Katika kikao hicho, Mhe. Mnzava aliwapongeza madiwani kwa ushindi wao katika uchaguzi na kuwashukuru wenyeviti wa vijiji kwa kushiriki kikamilifu katika kulinda amani wakati wote wa zoezi la uchaguzi, Alisisitiza kuwa mchango wao ulikuwa mkubwa katika kuhakikisha maeneo yao yanabaki salama na yenye mshikamano.
Aidha, aliwakumbusha viongozi hao majukumu yao ya msingi, hususan kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo, kwa kuzingatia maslahi ya wananchi waliowachagua.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mnzava alikemea vikali vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya mihuri katika maeneo yao, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha uaminifu wa wananchi kwa viongozi wao na kukwamisha haki. Akihitimisha kikao hicho, aliwataka madiwani na wenyeviti wa vijiji kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kuitunza amani iliyopo, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu ya jimbo na taifa kwa ujumla.


Post A Comment: