Na Benny Mwaipaja, Zanzibar


Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya afya kwa wananchi wake.

Mhe. Balozi Omar ametoa kauli hiyo wakati akizindua Kituo cha Afya cha Kisasa cha Kinduni, kilicho gharimu shilingi bilioni 3.77, kilichokojengwa katika Wilaya ya Kaskazini B mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema kuwa uwepo wa Kituo hicho cha Afya inathibitisha mafanikio makubwa katika sekta ya afya chini ya Uongozi wa Raisi wa Zanzibar wa Awamu ya nane, Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika ngazi zote za kijamii. 

“Serikali imeshajenga na kuweka vifaa katika  hospital 10 za wilaya katika wilaya za Unguja na Pemba, baada ya kuimarisha huduma katika ngazi ya wilaya zote, kuanzia mwaka 2023/2024 ambapo imeweka kipaombele katika kuimarisha miundombinu ya Afya ya msingi ili kutoa huduma bora zaidi ya Afya kwa jamii” alisema Mhe. Balozi Omar.

Alisema kuwa amefarijika kuona miundombinu ya afya inazidi kuimarika zaidi katika awamu ya nane ya Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kuwataka wananchi wakitunze  Kituo hicho ili kiwe chenye ubora na cha kuvutia siku zote ili kiendelee kutoa huduma bora za afya kwa muda mrefu na kuwahudumia Wananchi wengi zaidi.

Alisema kuwa Kituo hicho kitahudumia zaidi ya watu 19,546 wakiwemo watoto wenye umri wa chini ya mwaka mmoja 782, watoto wenye umri chini ya miaka mitano 2,834 na wanawake wenye umri wa kuzaa 5,336 kutoka shehia nne za Kinduni, Mkataleni, Mahonda na Mnyimbi pamoja na maeneo Jirani.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Kituo hicho cha afya Kinduni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Mgereza Mzee Miraji, alisema kuwa Mradi huo unajengwa kwa fedha za Serikali kwa gharama ya shilingi za Tanzania bilioni 3.77 chini ya Mkandarasi Mazrui Building Contractors Ltd na unasimamiwa na Mshauri elekezi, Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA).

Alisema Ujenzi wa kituo hicho unahusisha jengo moja la gorofa moja (G+2) na baada ya kukamilika kwake kitakuwa kinafanya kazi saa 24, kitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 30 kwa wakati mmoja na kitakuwa kikitoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo huduma za Kliniki na wagonjwa wa nje (OPD), huduma za Kliniki za mama na mtoto, maradhi ya pua, koo, masikio na macho, klinik ya magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari, Ngozi, kinywa na meno.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bw. Cassian Galoss Nyimbo, alisema kuwa Kitu cha Afya Kundini, ni cha kisasa kilichojengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa fedha zake za ndani, ambacho kitatoa huduma za afya karibu na wananchi na kwamba hawatakwenda umbali wa zaidi ya kilometa 5 kupata huduma hizo.

Nao wananchi wa Kundini na Mahonda, waliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwasogezea huduma za afya karibu nao kwa kuwajengea Kituo hicho kitakachotoa huduma za afya kwa mfumo wa kidigitali kwani tayari vifaa vya uchunguzi, matibabu na TEHAMA, vimeshafungwa.






Share To:

Post A Comment: