Magesa Magesa ,Arusha .



Arusha .Mkuu wa mkoa wa Arusha ,CPA Amos Makalla amewataka wananchi kuhakikisha kuwa wanajiunga na bima ya afya kwa wote ili waweze kupata vipimo,matibabu,na dawa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Ameyasema hayo jijini Arusha leo wakati akizindua sehemu maalumu ya kupokelea wagonjwa wa dharura pamoja na magonjwa yasiyoambukiza katika hospitali ya ALMC (Selian ) iliyopo jijini hapa .

Sehemu hiyo maalumu ya kupokelea wagonjwa hao imekarabatiwa na kuweka vifaa tiba na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)  ambapo ukarabati pamoja na vifaa tiba umegharimu kiasi cha shs 200 milioni .


CPA Makalla aliwapongeza wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kupata huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo yanayotolewa na Tasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete ambayo imeweka kambi ya matibabu hospitalini hapo .


"kila binadamu ni mgonjwa mtarajiwa hivyo nawapongeza wananchi kwa kuwahi kukua afya zenu, kwani kwa kufanya hivyo mtaweza kupata matibabu ya haraka na kuepukana na magonjwa hayo yasiyoambukiza."amesema CPA Makalla. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dokta Peter Kisenge amesema kuwa , Taasisi hiyo imekwisha  kufungua vituo sita katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kituo hiki.cha hapa  Arusha ambacho kitahudumia mikoa ya kaskazini na mikoa jirani .

Dkt Kisenge amesema kuwa , kambi hiyo ya  uchunguzi wa magonjwa ya moyo ilianza desemba 29 na inatarajiwa kifikia tamati  januari 9, na kusema kuwa hadi sasa zaidi ya wagonjwa 1,200 wameshahudumiwa na walioonekana na tatizo kubwa walipewa rufaa ya kwenda makuu ya Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. 


Amesema kuwa, mwitikio wa wananchi ni mkubwa hali inayoonyesha kuwa wananch9 wengi wanakabiliwa na tatizo la moyo na kuwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa siku hizo chache zilizobakia .


"Bado tatizo la magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni tishio kubwa kwa uhai wa mwanadamu hivyo umefika wakati sasa kwa wananchi kuchunguza afya zao mapema ili kuweza kutambua afya zao badala ya kusubiri  hadi dalili za ugonjwa husika kujitokeza kitendo ambacho kinakuwa ni changamoto kwenye suala la matibabu ."amesema Dkt Kisenge .

 Aidha ameshukuru hospitali hiyo ya ALMC (Selian) inayomilikiwa na kanisa la Kiinjili la.kilutheri Tanzania (KKKT)  pamoja na uongozi  wa kanisa hilo kwa kuwakubalia kuweka kituo cha kutoa huduma ya matibabu ya moyo katika hospitali hiyo kwani lengo la JKCI  ni kutaka kuona wananchi hawapotezi maisha  yao kwa tatizo la moyo.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ngarenaro, Abdulaziz  Chande (Dogo Janja) amemshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha JKCI ili kuweza kuja kutoa huduma hiyo kwa siku zote hizo kwa  wananchi wa Arusha  na mikoa ya jirani.

"Mimi.nina mfano ulio hai baba yangu mzazi anasumbuliwa na tatizo la moyo na ilikuwa nikitakiwa kumpeleka  jijini Dar es Salaam mara mbili kwa mwezi ,lakini kufunguliwa kwa kituo hiki mkoani Arusha kimeleta faraja sio kwangu tu ila kwa wananchi wote wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo kwani imewapunguzia gharama za kwenda kufuata huduma hiyo jijini Dar es Salaam. "amesema Dogojanja.

Share To:

Post A Comment: