Felix Zelote Afisa Usajili wa Dawa na Vifaa Tiba akitoa maelezo ya umuhimu wa kutoa taarifa za madhara na matukio yatokanayo na vifaa tiba na vitendanishi kwa wataalamu wa afya Mkoani Iringa.
Elizabeth Mollel Mkaguzi wa Dawa akieleza namna ya kutoa taarifa za madhara na matokeo yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi kupitia fomu zenye rangi ya chungwa na kwa namba ya simu bila malipo.


Na Fredy Mgunda,Iringa.

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba - TMDA imetoa elimu ya uhamasishaji juu ya utoaji wa taarifa za madhara na matukio yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi kwa watoa huduma za afya mkoa wa Iringa.

Akitoa elimu hiyo,Felix Zelote Afisa Usajili wa Dawa na Vifaa Tiba alisema TMDA inaendelea kutoa elimu ya uhamasishaji kuhusu utoaji taarifa za madhara na matukio ya vifaa tiba na vitendanishi kwa watoa huduma za afya ili wataalamu hao wa afya wanapobaini vifaa tiba vinaleta madhara kwa wagonjwa watoa taarifa TMDA.

“Tunataka watoa huduma za afya wanapobaini vifaa tiba vinaleta madhara kwa wagonjwa watoe taarifa TMDA lakini pia watoa huduma wa afya wanapobaini vifaa tiba havifanyi kazi inayotakiwa watoe taarifa ili TMDA tufanye ufuatiliaji”,ameeleza Zelote.

Zolete alizitaja njia za utoaji wa taarifa za madhara na matukio yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi ni kupitia Fomu maalumu ya rangi ya machungwa, kutumia simu ya kiganjani/mkononi kwa kubonyeza *152*00# kisha unafuata maelekezo pamoja kutoa taarifa kwa kupiga simu bure namba 0800110084

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa mkoa Iringa Mang’una  alisema kuwa elimu hiyo iwe msaada wa kutambua muda wa matumizi ya vifaa tiba huku akiwataka wananchi kuchukua tahadhari pale vitakapopatikana vifaa tiba vilivyokwisha muda wake.

“Vile vifaa tiba huwa vinakuwa na muda wa kutumia na muda huo ukishafikia basi vinatakiwa kutafutiwa njia ya kuhifadhiwa ili visitumike tena kutokana na madhara yake" Alisema Mang’una 


Mang’una amewataka Madaktari, Wafamasia, Wataalamu wa maabara, watunza vifaa tiba na mafundi sanifu wa vifaa tiba na vitendanishi kushirikiana na TMDA kwa kutoa taarifa za madhara na matukio yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi ili kuhakikisha jamii inakuwa salama muda wote.

Alimazia kwa kusema kuwa zoezi hilo linafanyika katika wilaya mbili za mkoa wa Iringa manispaa ya Iringa na mji wa Mafinga  huku TMDA ikitembelea vituo 12 vya vya afya vya serikali na binafsi

Dkt. Godfrey Mbagali ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Iringa na James Joseph ni mratibu utoaji wa taarifa za madhara na matukio ya vifaa tiba na vitendanishi Mkoani Iringa,walisema kuwa watafikisha elimu hiyo kwa jamii. 
walisema kuwa elimu hiyo itasaidia kutoa huduma iliyobora huku sababu ya athari za vifaa tiba visivyobora  ikiwa ni sababu ya kuanzisha kufikisha elimu hiyo

“Hii inatusaidia tuweze kutoa elimu bora na wito kwa watoa huduma wote kutoa taarifa kwenye vituo vya Iringa wakitoa hizi taarifa inatusaidia sisi kuwapa taarifa TMDA na kuweza kudhibiti hivi vifaa tiba ili vifaa viwe bora"alisema Mbangali

Nao watoa huduma za afya waliopatiwa elimu hiyo wameishukuru TMDA kwa kutoa elimu hiyo na kuahidi kuwa watashirikiana na TMDA kuifanya jamii kuwa salama kwa kutoa taarifa endapo watabaini vifaa tiba vinaleta madhara kwa wagonjwa ama havifanyi kazi kwa ufanisi unaotakiwa

Mafunzo hayo yalitolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa yakishirikisha Madaktari, Wafamasia, Wataalamu wa maabara, watunza vifaa tiba na mafundi sanifu wa vifaa tiba na vitendanishi.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: