Na Mwamvua Mwinyi,Rufiji

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahir Geraruma amewaasa, viongozi, watendaji na wataalamu wa Halmashauri kusimamia fedha za miradi na kujenga tabia ya kuhifadhi nyaraka za ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kujiepusha na mkanganyiko wakati wa ukaguzi.

Aidha amehimiza wananchi, kujitokeza katika Zoezi la Sensa agost mwaka huu kwa Ajili ya mipango ya maendeleo pasipo kupuuzia.

Akikagua miradi ya maendeleo katika mradi wa Zahanati ya Nyanda Katundu na barabara ya Mji Utete , wilayani Rufiji katika mbio za mwenge wa Uhuru Mkoani Pwani,Sahir aliwaasa watendaji hao kufuatilia miradi ya maendeleo kwa maslahi mapana ya wananchi kwenye Maeneo Yao.

Pia Sahir alikemea ,baadhi ya watumishi na viongozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani wanasababisha kudorora kwa miradi.

Akikagua mradi wa vijana kikundi cha Kumekucha Umwe Kaskazini, alielekeza Halmashauri kutenga fedha za vijana na kuhakikisha vikundi vinarejesha mikopo kwa wakati lengwa.

Akipokea mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Lindi ,mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, alifafanua, jumla ya nyumba 515,668 zimeingizwa kwenye mfumo wa Zoezi la anwani za makazi sawa na asilimia 105.61.

Alisema kufuatia maandalizi ya sensa na makazi wamejipanga na kuendelea kuhimiza wananchi kujitokeza kwenye Zoezi hilo agost mwaka huu.

“Mkoa wetu ulikuwa miongoni mwa mikoa 13 kwenye zoezi la sensa ya majaribio na Tunashukuru limefanya vizuri “Kunenge alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa,kiasi cha sh.milioni 816 .2 kutoka Serikali Kuu kimepokelewa na Halmashauri zimechangia milioni 320.

Pamoja na hayo, Kunenge alieleza mwenge wa uhuru ukiwa Mkoani hapo utapitia miradi 111 yenye gharama ya Zaidi ya Bilioni 69.2.

“Kati ya miradi hiyo miradi 25 itawekwa mawe ya msingi, 22 itazinduliwa,6 itafunguliwa na 58 kukaguliwa”alifafanua Kunenge.

Akipokea mwenge wa uhuru Mkuu wa wilaya ya Rufiji Edward Gowelle kutoka kwa Mkuu wa mkoa,alisema mwenge ukiwa Rufiji utapitia miradi sita yenye thamani ya milioni 600.5.

Kati ya miradi iliyotembelewa Rufiji ni pamoja na Zahanati Nyanda Katundu, barabara Mji Utete, mradi wa vijana kikundi cha Kumekucha Umwe Kaskazini, Mradi wa Uraghibishaji falsafa ya mwenge,ghala la mwananchi na madarasa ya Sekondari Mkongo.

Mwenge wa uhuru leo Mei 2 unatarajiwa kupokelewa huko Mkupuka wilaya ya Kibiti.

  




Share To:

Post A Comment: