Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia, Profesa Adolph Mkenda, akiangalia bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa kutokana na mabaki ya mazao zilizotokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU), alipokwenda kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.


.Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia, Profesa Adolph Mkenda, akisikiliza maelezo kuhusu ramani mbalimbali zinazotumiwa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU), katika kufundishia alipokwenda kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda akimsikiliza Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Mazingira wa Chuo Kikuu Ardhi (ARU), akieleza kuhusu bidhaa zilizotengenezwa kutokana na mabaki mbalimbali wakati alipokwenda kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolph Mkenda, amekipongeza Chuo Kikuu Ardhi (ARU), kwa namna kilivyofanikiwa kufanya tafiti mbalimbali zenye tija ambapo matokeo ya tafiti hizo zimesababisha kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kujipatia kipato na pia kutatua changamoto za maswala ya ardhi, makazi na mazingira.

Ametoa pongezi hizo leo Machi 9, 2022 wakati akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi unaoendelea jijini Dar es Salaam.

Amesema chuo hicho kimeweza kuwatumia wasomi wake kufanya tafiti nyingi ambapo nyingine zimeweza kuja na bidhaa ambazo iwapo zitafanywa kibiashara zaidi zinaweza kukiingizia chuo mapato mengi na kuvitaka vyuo vingine kuiga ubunifu kama huo.

“Nakipongeza pia chuo hiki kwa kujenga uhusiano na Shirika la kimataifa la maendeleo la Swedeni (Sida) hali ambayo imewezesha watanzania watafiti kupata ufadhili wa kufanya tafiti na wengine kwenda kusoma nchini humo,” amesema

Amesema kwenye bajeti ijayo serikali itatenga fedha nyingi kwa ajili ya tafiti na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi watanzania kwenda kusoma fani mbalimbali nje ya nchi.

Amesema pamoja na ukweli kwamba serikali itatenga fedha za utafiti na ufadhili wa wanafunzi, vyuo navyo vinapaswa kujenga uhusiano na vyuo vingine duniani na taasisi mbalimbali ili kupata miradi mbalimbali.

Amesema Mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa na Mwenyekiti wa Baraza la chuo, Balozi Salome Sijaona wamejitahidi kujenga uhusiano mzuri na vyuo mbalimbali duniani.

“Mimi ningependa kuona juhudi zinazofanyika hapa zinafanywa na vyuo vingine.

Ameongeza kuwa, wale mapofesa wanaoweza kuandika maandiko yatakayowashawishi wafadhili kutoa hela kwa vyuo vyao na kusaidia kuendeleza vyuo hivyo walindwe badala ya kunyanyaswa.

Profesa Mkenda amesema iliwahi kutokea kwenye mradi mmoja ambapo mradi ulikuwa unasomesha watanzania na kununua makaratasi na mashine za kudurufia lakini watu wakataka kukata kodi kwenye mradi huo.

“Nadhani si sahihi kutoza kodi kwenye vitu vya msaada kwa sababu wenyewe wanaweza kuondoa na hata kupeleka kwenye vyuo vingine kama Makerere na kwingineko ambako hawatozi kodi na vikwazo vingine tuviondoe ili kuvutia miradi mingi ya msaada kwenye vyuo”

Amesema maprofesa kwenye vyuo mbalimbali duniani wamekuwa wakiandika miradi ya kuvutia wafadhili na miradi hiyo imekuwa ikipata fedha na kuwa mkombozi mkubwa kwa maendeleo ya vyuo hivyo.

“Vyuo vyote duniani havitegemei fedha za serikali tu bali kupitia miradi inayoandikwa na maprofesa wao, wanafanya hivyo Afrika Kusini, Misri, Marekani na Sweeden hivyo hakuna sababu ya Tanzania kushindwa kuandika miradi,” amesema

Amesema kinachotakiwa ni vyuo kuwawekea mazingira wezeshi ili kutimiza azma yao badala ya kuwawekea vikwazo na hata wanapotaka kusafiri kwenda nje ya nchi waruhusiwe .

Naye Naibu Makamu Mkuu wa chuo Taaluma , Pofesa Gabriel Kassenga amesema mkutano huo unashirikisha wadau kuhusu tafiti zilizofanywa na ARU kwa kushirikiana na Sida kwa miaka mitano iliyopita 2017-2022.

Amesema mkutano huo unawashirikisha wataalamu wa masuala ya ardhi, mabadiliko ya tabia nchi na mazingira ili kubadilishana mawazo kuhusu matokeo ya utafiti huo yatakavyoboresha sera za ardhi na mabadiliko ya tabia nchi .
Share To:

Post A Comment: