Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Na Dotto Kwilasa, DODOMA.

SERIKALI kupitia Wizara ya afya imewatahadharisha maofisa wake wa mipakani wanaotoa vyeti bandia vya chanjo ya homa ya manjano kuacha mara moja tabia hiyo na kwamba kwa yeyote atakayegundulika atashughulikiwa.

Hatua hii imekuja kufuatia kuwepo kwa tetesi za uwepo wa ugonjwa huo ambapo mnamo tarehe 03 Machi, 2022 Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo hapa nchini, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Kenya katika Kaunti ya Isiolo umbali wa takribani Kilomita 285 (Kaskazini mwa Nairobi) . 

Hayo yamesemwa leo Machi 9,2022 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dodoma  ambapo amesema kuhusu tahadhaki ya mlipuko wa ugonjwa huo na kuelezwa kuwa maafisa hao wamekuwa na taabia ya kutoa vyeti feki vinavyo mtambulisha  mtu kuwa amechanja kumbe hajachanja.
 
Ameeleza kuwa taarifa hiyo ilieleza kuwa, mgonjwa wa kwanza mwenye dalili za ugonjwa huu alipatikana mnamo tarehe 12 Januari 2022 na hadi kufikia tarehe 03 Machi 2022, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 15 na vifo vitatu (3) vilivyotokana na ugonjwa huu hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuchukua tahadhari. 

Kadhalika Waziri Ummy amefafanua kuwa kati ya sampuli sita (6) zilizopimwa katika maabara ya Kenya (KEMRI), sampuli tatu (3) zilithibitika kuwa va virusi vya homa ya Manjano kwa kutumia vipimo vya serology na PCR. Vilevile, kumekuwa na tetesi za kuwa na wagonjwa wenye dalili za homa ya Manjano katika nchi za Uganda, Sudan ya Kusini na Chad.

"Nchini kwetu taarifa za kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele wa (Integrated Disease Surveillance and Response-IDSR) zinaonesha kuwa hapajakuwepo na taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano,

Vile vile katika kipindi hiki, mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji wa tetesi za magonjwa haujaashiria kuwepo kwa dalili za ugonjwa huo hapa nchini. Hata hivyo, ninatoa tahadhari kwa wananchi ili kuchukua hatua na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini kwetu,"alisema.

 Aliongeza kuwa ugonjwa wa Homa ya Manjano husababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes, kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na vilevile kati ya mtu na mtu na kwamba watu wanaofanya kazi kwenye misitu huweza kuambukizwa kwa kung’atwa na mbu ambao hupata vimelea vya ugonjwa huo kutoka kwa wanyama wa porini kama Nyani na huambukizwa kati ya mtu na mtu pindi mtu mwenye virusi hivyo anapoumwa na mbu na hatimaye kueneza kwa mtu mwingine. 

Alizitaja dalili za ugonjwa wa Homa ya Manjano kuwa  ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni na wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi.

"Dalili hizi huanza kuonekana katika Kipindi kati ya siku 3 hadi 6 baada ya kuambukizwa, hauna tiba mahsusi bali mgonjwa anayezidiwa uhitaji huduma ya karibu, ambapo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zinazojitokeza lakini pia mara nyingi matibabu yanahusisha utoaji wa dawa za kushusha homa na kupunguza maumivu au kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kwa kuwekewa dripu,"alifafanua 

Sambamba na hatua hizo,Waziri Ummy alisema Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu wasafiri wote wanaoingia nchini hususani kutoka nchi zilizo katika hatari ya maambukizi ya homa ya manjano,kuhakikisha kuwa chanjo za kutosha za ugonjwa wa Homa ya manjano zinakuwepo hapa nchini.

Hatua nyingine ni kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira ili kudhibiti mazalia ya mbu,kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo na kuwaasa wananchi kuzingatia kutoa taarifa mapema katika vituo vya kutolea huduma ya afya pale wanapoona mgonjwa mwenye dalili za homa hiyo

"Wizara inapenda kuwakumbusha watanzania kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa,kutilia mkazo usafi wa mazingira na kuzuia maji yasituame ovyo kwenye mazingira tunayoishi ili kuangamiza mazalia ya mbu katika maeneo yanu,..

 Kwa wasafiri wanaokwenda nje ya nchi, wahakikishe wamepata chanjo dhidi ya homa ya manjano (Yellow Fever),huduma za chanjo hiyo zinapatikana katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere (Dar es Salaam), Hospitali ya Mnazi Mmoja, Ofisi za Afya Bandari (Dar es Salaam) na kituo cha Afya cha IST (Dar es Salaam) pamoja na Ofisi za Afya za mipakani,"alisisitiza.

Kwa upande wake Mwakilishi mkazi wa Shirika la afya duniani nchini Tanzania (WHO)ameeleza kuwa ugonjwa huo unazuilika kwa njia ya chanjo ambayo kutokana na ushauri wa Shirika hilo hutolewa kwa wasafiri hasa wanaokwenda katika nchi zile ambazo zimekuwa na ugonjwa huo ili kuwazuia wasafiri hao wasipate ugonjwa na kuingiza katika nchi zao pindi wanaporejea. 

Alisema  pamoja na utoaji wa Chanjo kwa wasafiri, ufuatiliaji wa kina umekuwa unafanyika kwenye mipaka ili kuhakikisha kuwa wasafiri wanaoingia kutoka katika nchi zilizokwishakuwa na ugonjwa huu wana vyeti vinavyoonesha kuwa wamepata chanjo hiyo.  
"Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania haijawahi kuwa na taarifa ya mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Homa ya Manjano tangu mwaka 1950",amesema

Baada ya kupata taarifa za ugonjwa huo katika nchi ya Kenya, Shirika letu linaendelea kuchukua hatua zote stahiki ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa watu wenye dalili za ugonjwa katika vituo vya Afya vya bandari, viwanja vya ndege na mipakani kwa wasafiri watokao nje ya nchi na kuhakikisha kuwa wasafiri watokao nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanakuwa na uthibitisho wa chanjo ya Homa ya manjano,"alisema Mwakilishi huyo wa WHO.

Akitahadhalisha kwamba ugonjwa huo upo jirani lakini lakini ni rahisi kuzuiliks hivyo kuwataka wananchi kuwa watulivu na kusikiliza maelekezo na ushauri utakaotolewa na wataalam wa Afya katika maeneo yao au vyombo vya habari.

Pamoja na hayo alieleza kuwa WHO inaendelea kutoa wito kwa wadau katika ngazi zote kuendelea kushirikiana na Serikali  katika kutekeleza jitihada mbalimbali za kupambana na magonjwa ya milipuko ikiwepo ugonjwa huo ili kuwe na wananchi wenye afya njema na kuwezesha shughuli za uzalishaji kuendelea.
Share To:

Post A Comment: