Wajumbe wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho Fatma Mode wamefanya ziara ya kutembelea viwanja ambavyo Chuo hicho kinatarajia kujenga kampasi zake katika Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Njombe.

Wakiwa katika ziara hiyo Viongozi hao walikagua maeneo yote na kuahidi kuyaendeleza kwa Maslahi Mapana ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.

Baada ya kutembelea eneo lililiopo Chidachi- Ntyuka mkoani  Dodoma lenye ekari 50 na lile lililopo kata ya Maguvani halmashauri ya Mji - Makambako lenye ukubwa wa ekari 103.2, Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Fatma Mode amesema ameridhishwa na hali za viwanja sasa kinachotakiwa ni kujenga.

“Tumeona maeneo yote ni mazuri, tumejiridhisha  sasa kinachofuata ni kujenga kwa lengo la kuongeza kampasi na kupanua wigo wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa na kampasi katika mikoa mbalimbali hapa nchini,”Alisisitiza Makamu Mwenyekiti Fatma Mode.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Prof. Haruni Mapesa amesema kwa sasa Chuo kinaandaa mpango kazi wa ujenzi ili mpango kazi huo uwasilishwe kwenye bodi ya Chuo na kuwa ndani ya miaka mitatu ujenzi utaanza kwa kujenga Madarasa na ofisi za Utawala katika halmashauri ya Mji - Makambako.

Prof. Mapesa ameishukuru Halmashauri ya Mji- Makambako kwa kutoa eneo bure kwa ajili ya Chuo, ambapo ameahidi kuliendeleza.

Prof. Mapesa amesema kwa sasa Chuo kina Kampasi tatu ikiwemo Kampasi ya Kivukoni iliyopo jijijini Dar es Salaam, Kampasi ya Karume- iliyopo Zanzibar, Kampasi ya Pemba iliyopo ChakeChake Pemba.

Mkuu huyo wa Chuo ameainisha maeneo ambayo Chuo inatarajia kuwa na kampasi ni pamoja na Mkoa wa  Tabora,Njombe, Dodoma, Mwanza, Arusha  na Katavi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Njombe Juma Sweda amesema kujengwa kwa kampasi ya Chuo cha Kumbukumbu Mwalimu Nyerere katika mji wa Makambako ni jambo jema na maamuzi ya kuchagua eneo  la makambako ni sahihi sana kwa kuwa eneo hilo lina mwingiliano mkubwa wa shughuli mbalimbali za Kimaendeleo.

Hata hivyo Mgombea Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi ( CCM) wa Jimbo hilo Daniel Chongolo amesema Wananchi wa Makambako wako tayari muda wowote kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo mara tu Chuo kitakapoanza ujenzi kwa lengo la kuleta Maendeleo.

“Sisi wananchi wa Makambako tunakipongeza sana Chuo kwa maono na maamuzi ya kuchagua Makambako na kujenga Kampasi ya Chuo hapa, ni heshima maana Jina la Chuo limebeba Jina la baba wa Taifa hivyo tunaamini kabisa Maono na Falsafa zote za baba wa Taifa zitawanufaisha sana Vijana watakaosoma katika Kampasi hiyo na Wadau wengine wa Elimu wa Makamabako nao watanufaika pia,” Alisema Chongolo.

Imeandaliwa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko;
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
22.10.2022
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: