Viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi wilayani Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya makabidhiano ya madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi kwenye shughuli za kukabidhi madawati.


Afisa Maendeleo Wilaya ya Ikungi  Haika Masawe akizungumza jambo kwenye hafla hiyo.
Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi, Yahaya Njiku ambaye pia ni mdau wa maendeleo akizungumza kwenye halfa hiyo ya kukabidhi madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Wananchi wa Kijiji cha Mwisi wakiwasikiliza kwa makini viongozi kwenye halfa hiyo.

Madawati yakikabidhiwa. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Lighwa Borgius Ntandu.

 Saimon Philipo mmoja wa vijana waliochangia madawati hayo akielezea namna walivyoguswa na kuamua kutoa msaada wao.

Viongozi wakiwa meza kuu.Na Dotto Mwaibale, Singida.


VIJANA wazalendo kutoka Kijiji cha Mwisi Kata ya Lighwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa Madawati kwenye Shule ya Msingi Mwisi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye madawati wakati wa masomo yao.

Vijana hao ambapo kwa sasa wako maeneo mbalimbali,wameona vema kuunga mkono juhudi za Serikali na wameamua kuanzia nyumbani kwenye Shule walikosomea ambapo wamechangia madawati 37.

Akikabidhi Madawati hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi amewapongeza Vijana hao ambapo amesema amefarijika kuona wazalendo wanaokumbuka kurudisha fadhila nyumbani.

"Hongereni sana ni watu wachache sana wanaokumbuka kurudisha fadhila,hivyo endeleeni kuchangia mnapoona kuna changamoto katika kijiji chenu.Na mimi nachangia madawati 20." alisema Kijazi na kuongeza.

"Vijana kwenye risala yenu mumesema kuna uhitaji wa kukarabati chumba cha Darasa katika Shule hii ambalo litatumika kama Ukumbi, nachangia mifuko 30 ya Saruji pamoja na kumlipa fundi,hivyo mtakapoanza mipango niambieni." alisema.

Kijazi aliwataka Vijana kubuni Miradi mbalimbali ili kufungua fursa za ajira zitakazopelekea maendeleo ya Elimu na mambo mengine ambapo aliwaahidi kuwa Halmashauri kupitia asilimia 10%  zinazotengwa itatoa mikopo hiyo kwa Vijana watakao anzisha miradi ya maendeleo.

Aidha mmoja wa vijana hao waliounda umoja wa wanadarasa waliohitimu Shule ya Msingi Mwisi Mwaka 2007,Saimon Philipo alisema waliona zawadi pekee ya kulipa nyumbani ni kutengeneza madawati ili wadogo zao wasome kwenye mazingira mazuri.

"Sisi tuliamua kuanzisha umoja wetu ili tuweze kuchangia shughuli za maendeleo,Sio tu hapa tutafanya hata maeneo mengine lakini tuaona tuanzie kwanza nyumbani." alisema Saimon.

Naye Diwani wa Kata hiyo Borgius Ntandu aliwataka Vijana wa Kata hiyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuiga mfano wa Vijana wengine wazalendo wanaunga mkono juhudi za Serikali.

Hata hivyo Diwani huyo aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Mwisi kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake Mdau wa maendeleo wilayani humo Yahaya Njiku ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi alisema uzalendo wa vijana utapimwa kwa utendaji kazi wao na sii vingine,hivyo akawaomba vijana wengine kuwa wazalendo kwa kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

"Huyu Saimon mmoja waliochangia madawati haya nimesoma naye kidato cha tano na sita na amekuwa rafiki yangu sana,nimeona nimuunge mkono katika hili na hata mengine.Nachangia sh.elfu Hamsini." alisema Njiku. 

Share To:

Post A Comment: