Articles by "KIMATAIFA"
Showing posts with label KIMATAIFA. Show all posts

   




Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la waasi la M23 wanatazamiwa kufanya mazungumzo ya kwanza ya moja kwa moja leo mjini Doha, Qatar, hatua muhimu katika mchakato wa kuhitimisha mzozo mkongwe mashariki mwa DRC unaoendela kwa miongo kadhaa.


Mazungumzo haya yanakuja wakati ambapo hali ya kibinadamu katika maeneo ya mashariki mwa Kongo inazidi kuwa mbaya, huku maelfu wakipoteza maisha na zaidi ya watu milioni moja kulazimika kuyakimbia makazi yao tangu mapigano kushika kasi mwanzoni mwa mwaka huu.


DRC, Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda zinaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono M23 kwa kuwapatia msaada wa kijeshi na silaha, tuhuma ambazo Rwanda imekuwa ikikanusha vikali.


Wakati wa shughuli ya kitaifa ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, Rais Paul Kagame hakuzitaja nchi moja kwa moja lakini alisisitiza kuwa matalfa hayo yanapaswa kuyatatua matatizo yao na kumwacha yeye ashughulkie ya kwake.


Kwa muda mrefu, jitihada za kidiplomasia zimesuasua. Mwaka jana, mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Angola yalivunjika baada

ya Rwanda kushinikiza mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya DRC na kundi la M23.


Siku moja baada ya M23 kutangaza kujiondoa kwenye mazungumzo hayo, Rais Felix Tshisekedi wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda walikutana ana kwa ana nchini Qatar kwa mara ya kwanza, mpatanishi akiwa ni Amir wa Qatar. 


Mazungumzo hayo yalichochea mwamko mpya wa kidiplomasia, na hivyo kufanikisha mashauriano yanayoanza rasmi leo.

 




Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametangaza kuwa wanajeshi wa Ukraine wamewakamata raia wawili wa China waliokuwa wakipigana upande wa Jeshi la Urusi katika mkoa wa Donetsk, hatua ambayo imeibua maswali kuhusu nafasi ya China katika mozo huo unaoendelea.


Zelensky amesema kuwa hii ni dalili kuwa "idadi ya Wachina katika Jeshi la Urusi ni kubwa zaidi kuliko inavyodhaniwa." Kauli hiyo imekuja wakati ambapo China imekuwa ikijitambulisha kama mpatanishi wa amani kwenye mzozo huo, huku ikiendelea kuimarisha uhusiano wake wa karibu wa kiuchumi na kisiasa na Urusi.


Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Ukraine, Andrii Sybiha, amesema amesikitishwa na taarifa hizo na kuhoji msimamo wa China kuhusu amani, akiongeza kuwa ubalozi wa China nchini Ukraine umeombwa kutoa maelezo rasmi kuhusu sababu za raia wake kuonekana mstari wa mbele kwenye mapigano dhidi ya Ukraine.


Hii ni mara ya kwanza kwa Ukraine kutoa taarifa rasmi inayohusisha raia wa China katika uwanja wa vita kama wapiganaji upande wa Urusi. Hadi sasa, Urusi na China bado hawajatoa majibu rasmi kuhusu tuhuma hizo.


Aidha, Kyiv na baadhi ya maafisa wa Magharibi pia wanadai kuwa Korea Kaskazini imetuma maelfu ya wanajeshi kusaidia juhudi za kijeshi za Urusi, hali inayoibua hofu ya kuongezeka kwa ushawishi

wa mataifa rafiki wa Moscow katika mzozo huo.


Kwa muda mrefu, China imekana kuipatia Urusi msaada wa kijeshi, huku ikisisitiza msimamo wake wa kutotegemea upande wowote.


Lakini tukio hill linazua maswali kuhusu uhalisia wa msimamo huo.


Wakati hayo yakijiri, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi yameripotiwa usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi katika miji ya Dnipro na Kharkiv chini Ukraine, yakiwajeruhi watu 14 na kusababisha visa kadhaa vya moto.


Kwa sasa, Urusi inadhibiti karibu asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine, huku mapigano yakiendelea kushika kasi, hasa katika maeneo ya mashariki.



Na Christina Thomas , Morogoro. 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani amekipongeza Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo SUA Kwa kufanya Tafiti zenye tija katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kuongeza uchumi wa Watanzania kupitia sekta hizo.

Ametoa pongezi hizo Agosti 2, 2024 wakati akifungua Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi".

Dkt. Buriani amesema SUA imetumia mabadiliko ya tabianchi kama fursa kwa kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuendeleza kilimo nchini 

Aidha amewataka wakulima na wafugaji kutumia fursa ya maonesho hayo kwa kutembelea  Maonesho ya nanenane  kujifunza vitu vipya kama nyasi za malisho, teknolojia ya upimaji wa udongo, miundombinu ya umwagiliaji kwani nchi haijaweza kutumia fursa kikamilifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha ukame, mafuriko na kuongezeka kwa joto.

Pia amewapongeza wakulima na wavuvi ambao wamejitoa kushiriki Maonesho ya Nane Nane mwaka huu na kusema kuwa ushiriki wao utasaidia kuongeza ujuzi, uwezo na mawazo tofauti kutokana na kukutana na wadau wengine kupitia maonesho hayo kama lengo lake la kutoa elimu na kuongeza wafugaji na wavuvi na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.

Kwa upande wao wananchi waliopata fursa ya kutembelea mabanda na kijifunza teknolojia za Kilimo, mifugo na Uvuvi wamesema wamepata elimu itakayowasaidia katika shughuli zao za Kila siku.

 


Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Wakazi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Wilaya Mtwara Vijijini wamefurahishwa na uamuzi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakuitaka Bandari ya Mtwara kuanza  kusafirisha  korosho.

Akizungumza leo wilayani humo katika mahojiano maalum na Afisa wa Idara ya Habari -MAELEZO,  Mkazi wa Nanyamba na Mkulima wa korosho, Bw. Burhan Mwema anaeleza kuwa uamuzi huo wa Rais Samia utawanufaisha zaidi wakulima kwa kuwa awali iliwapa ugumu  kusafirisha korosho kwa kutumia Bandari ya Dar es salaam.

" Napongeza sana Mhe. Rais kwa hili, itatusaidia sisi hata kujua kinachoendelea kuhusu korosho zetu, kwa kuwa tutaona kila kitu kuliko ilivyokuwa inaenda huko mbali".

Mkulima wa korosho,  Ahmed Mchila anasema "Kwanza nimefurahishwa na uamuzi huu wa kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha korosho, hii bandari ipo karibu nasi hapa tutaweza kufuatilia kwa karibu zaidi kila kinachoendelea. Pia, kusafirisha kwa bandari yetu itasaidia hata uzito kutopungua tofauti na tukipeleka mbali muda unavyotumika zaidi katika kusafirisha na korosho zetu zinapungua uzito na bei pia inapungua". Amebainisha Mchila.

Naye, Mbaraka Said anasema  " Kusafirisha korosho kupitia bandari yetu hapa itasaidia kuchochea uchumi wa Mtwara kwa kuwa hata wanunuzi kutoka mbali watafika na wakiwa hapa watafanya shughuli mbalimbali zitakazochochea uchumi wetu"

Aidha, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan jana akizungumza na wananchi wa Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona ameeleza "Nimeona eneo jipya la bandari ambalo limejengwa na Serikali. Bandari ile haijajengwa kupamba Mji wa Mtwara. Bandari ile imejengwa kutoa huduma za usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, kutoka Mtwara na kuingia Mtwara".

"Kilio chenu wananchi ni suala la korosho, kwamba korosho sasa isafirishwe kutokea Bandari ya Mtwara. Mimi sielewi ni nini kinawazuia Mtwara kutosafirisha pale Korosho". Amebainisha  Mhe Rais Samia.

Amesisitiza "Niwaombe sana Wanamtwara hasa viongozi, yale ambayo yalikuwa yanazuia Korosho kusafirishwa kupitia bandarini kaeni  mkubaliane. Najua kuna wafanyabiashara wenye malori ambayo ndio wanapakia korosho kupeleka Mjini au Dar es Salaam. Lakini kuna wenye vituo vya mafuta, korosho ikisafirishwa kwa meli hawatapata fursa ya magari kujaza mafuta".

Mhe. Rais Samia ameendelea na ziara yake mkoani Mtwara, ambapo mapema leo amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara eneo la Nangururuwe na Nanyamba na kisha kuelekea Uwanja wa Majaliwa Tandahimba  kwa ajili ya kuzungumza na wanachi wa eneo hilo.


 Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amevitaka vikundi vya Ulinzi na Usalama vinavyoshiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kwa majeshi ya nchi za Afrika ya Mashariki kuhakikisha vinaliwakilisha vema taifa la Tanzania ili kujenga ushirikiano mzuri na nchi jirani.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa zoezi hilo linalofanyika katika mji wa Musanze, Rwanda, Jenerali Mkunda alisema kuwa zoezi hilo liwe chachu ya kujifunza namna ya kutatua changamoto za kiulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa wananchi wanayategemea zaidi majeshi yao kuwapatia msaada wa ulinzi na uokozi pindi majanga yanapotokea.

“Unajua hakuna kitu kikubwa ambacho huwa kinarudisha na kujenga imani ya wananchi kwa majeshi yao kama kupewa msaada wa kijamii pindi wapatapo majanga. Imani yao kubwa hubaki kwa wanajeshi ambao ndio huwa wa kwanza kutoa msaada.” Alisema Jenerali Mkunda.

Jenerali Mkunda pia amevitaka vikundi vinavyoshiriki kwenye zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kudumisha udugu na ushirikiano wa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

“Nchi yetu ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikisifika kwa kuwa marafiki wa kweli katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na dunia nzima, hivyo hakikisheni mnaendelea kuwa mfano wa kuigwa”, alisisitiza Jenerali Mkunda.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa zoezi hilo kwa taasisi na mamlaka za kiraia, Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Gerson Msigwa alisema kuwa huu ni wakati muafaka wa kufanya kazi pamoja kwani pindi majanga yanapotokea, mamlaka mbalimbali zinahusika kutoa utaalam wa kukabiliana na majanga hayo.

“Tupo tayari kufanyakazi na Majeshi ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha  kuwa tunatekeleza majukumu yetu ya kihabari kusaidia kufanikisha majukumu ya kulinda amani na kurudisha imani ya wananchi pale majanga yanapotokea”, alisema Bw Msigwa.

Zoezi hilo la wiki mbili limefunguliwa rasmi Jumapili na Waziri wa  Ulinzi wa Rwanda Mhe. Juvenal Marizamunda    ambaye alimkabidhi Bendera ya kuashiria kuanza kwa zoezi Mkuu wa Zoezi hilo Dk. Alice Urusaro Uwagaga Karekezi ambaye naye alikabidhi bendera hiyo kwa Mkuu wa Majeshi ya Kikanda ( REMIKA)  Brigedia Jenerali Julius Gambosi.

Zoezi linalenga kuvijengea vikundi vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za kiraia uwezo wa kukabiliana na  Ugaidi,Uharamia, Menejimenti ya Majanga pamoja na Ulinzi wa Amani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Washiriki wa zoezi hilo ni pamoja na Majeshi ya Ulinzi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Kituo cha Taifa cha kukabiliana na Mapambano dhidi ya Ugaidi. Aidha, Taasisi za Kiraia zilizoshirikishwa ni pamoja  na zilizo chini ya  sekta za Habari, Haki za Binaadam, Usawa wa Kijinsia pamoja na Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

MWAKILISHI wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Aristides Mbwasi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.


Na Alex Sonna-DODOMA


SERIKALI imezindua mashindano ya tuzo za ubora kwenye huduma na bidhaa zenye lengo la kuhakikisha mifumo,bidhaa na huduma zinakidhi ubora kitaifa,kikanda na kimataifa ili kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote.


Tuzo hizo ambazo zitakuwa katika vipengele vitano ni pamoja na kwa kampuni bora ya mwaka,bidhaa bora ya mwaka,huduma bora ya mwaka,muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya bora.


Hayo yameelezwa leo Oktoba 27,2022 Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji,Viwanda na Biashara,Aristides Mbwasi wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023.


Mbwasi amesema tuzo za ubora zilianzishwa ikiwa ni makubaliano baina ya wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ili kutambua na kukuza sekta ya biashara kupitia ubora wa biadhaa na huduma katika ukanda huo.


“Kwa sababu hiyo.serikali kupitia Wizara ya Uwezekezaji,Viwanda na Biashara iliona umuhimu wa kuanzisha tuzo za ubora za kitaifa na kutoa jukumu kuziratibu kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS)


“Kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSP) Taasisi za Viwango Zanzibar (ZBS) Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo nchini (SIDO) Chama cha Wanawake wafanyabiashara Tanzania (TCCIA) na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).


Amesema tuzo hizo ni sehemu ya mipango ya serikali katika kuboresha huduma na bidhaa zinazotengenezwa nchini kupitia matumizi ya viwango na kanuni za ubora kwa taasisi za umma na binafsi.


Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa mifumo bidhaa na huduma zinakidhi ubora kitaifa,kikanda na kimataifa na hivyo kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote.


Mbwasi amesema tuzo hizo zimegawanyika katika vipengele vitano ambavyo ni Tuzo kwa kampuni bora ya mwaka,tuzo kwa bidhaa bora ya mwaka,tuzo huduma bora ya mwaka,tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi na mtu mmoja mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya bora.


“Kwa kipengele cha kwanza hadi cha nne zimeandaliwa tuzo kwenmye makundi mawili kwa kila kipengele yaani tuzo kwa kampuni kubwa na pia tuzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.


Aidha kipengele cha tano kinahusisha tuzo kwa mtu mmoja pekee ambaye atakuwa ni yule aliyefanya vizuri kwenye masuala ya ubora.


Amesema washindi si tu watapata nafasi ya kufahamika pia watapata fursa ya kushiriki kwenye mashindano ya tuzo za ubora kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia katika mashindano ya tuo za ubora za nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Mbwasi amesema washindi wa tuzo za ubora mwaka uliopita walishiriki katika mashindano ya kikanda katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC Qualty Award) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC Qualty Award.


“Katika mashindano hayo kampuni kutoka Tanzania zilizonyakua tuzo ni Kampuni kubwa bora ya mwaka EAC Said Salim Bakhresa Company Limited,bidhaa bora ya mwaka EAC Faima Production na huduma bora ya mwaka kwa SME EAC –Caps Tanzania Ltd.


“Mataukio haya ni makubwa na yanatoa fursa kwa bidhaa na huduma zinazotolewa hapa nchini kuaminiwa zaidi hata nje ya mipaka ya Tanzania hivyo kupanua wigo wa masoko kwa bidhaa na huduma,”amesema.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt Yusuph Ngenya,amesema kuwa maandalizi yanaendelea vizuri kwa kutumia warsha mbalimbali na vyombo vya habari ,mitandao ya kijamii ambapo yatasaidia kuwapata washindi.


"Katika maandalizi haya tumewapa kipaumbele akina mama wajasiliamali kuwahamasisha ili waweze kushiriki kwani ni wengi ambao wamejikita kwenye ujasiliamali." amesema Ngenya.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango ambaye amemwakilisha Mkrugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS)Bi.Hafsa Ali Slim,amesema kuwa wanatarajia kutoa uelewa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi.




Mkurugenzi Mkuu Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt Yusuph Ngenya,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.




Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Viwango ambaye amemwakilisha Mkrugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Zanzibar (ZBS)Bi.Hafsa Ali Slim,akielezea jinsi walivyojipanga kutoa elimu kwa upande wa Zanzibar ili waweze kushiriki kwa wingi zaidi kuhusu tuzo za ubora za kitaifa kwa mwaka 2022-2023


Mahakama katika mji mkuu wa Uganda Kampala imemhukumu kifungo cha maisha jela mfanyabiashara wa pembe za ndovu. Pascal Ochiba alikamatwa Januari mwaka huu akiwa na vipande viwili vya pembe za ndovu vyenye uzani wa karibu kilo 10. Hakimu alisema kuwa Bw Ochiba alikuwa amerudia kosa kwa mara nyingine na anastahili adhabu ya juu zaidi, kwa ulinzi wa siku zijazo wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka. Mnamo Julai 2017, Bw Ochiba alikamatwa akiwa na vipande vinne vya pembe za ndovu na ngozi ya okapi na kupelekwa gerezani. Okapi ni wanyama adimu wa msituni wenye alama kama pundamilia na wanapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, Sam Mwandha, alielezea uamuzi huo kama mafanikio ya kihistoria katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori. Mnamo mwaka wa 2019, nchi ilipitisha sheria ya kifungo cha maisha kwa watu wanaopatikana na hatia ya ujangili au usafirishaji wa wanyama walio hatarini kutoweka. Kuna tembo zaidi ya 7,900 waliobaki porini nchini Uganda, na wanyama hao wako hatarini kutoweka. #CHANZO:BBC


 RAIS wa Jamhuri ya Kenya Willima Ruto amesema wanawashukuru watanzania wote kwa namna ambavyo waliwaombea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa nchi yao na hivyo uchaguzi umefanyika kwa amani na wenye demokrasia.


Ruto ameyasema hayo leo Oktoba 10,2022 katika Ikulu ya Dar es Salaam wakati akizungumza mbele ya Rais Samia , maofisa wa nchi za Tanzania na Kenya pamoja na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kutoa shukrani kwa Watanzania kwa kuwaombea na hatimate wamefanya uchaguzi wa demokrsia.

“Tunawashukuru sana Watanzania kwa kutuombea kutujali, na kuonesha upendo wenu mkubwa kwetu wakati wote wa uchaguzi wetu kule Kenya,tunafahamu mlituombea na mliunga nasi, tunashukuru sana.Uchaguzi wetu umefanyika kwa amani na utulivu , tulikuwa na dekrasia na uchaguzi uliwazi, tunawashukuru,’amesema Rais Ruto na kuongeza “Ahsanteni sana kwa kutuombea ili tuwe na uchaguzi wa demokrasia, uchaguzi wa amani.

Awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kabla ya kumkaribisha Rais Ruto kuzungumza na waandishi wa habari, ametumia nafasi hiyo kuelezea amemshukuru Rais Ruto kwa kukubali kuitikia wito na kuja, hivyo amemkaribisha nchini.

“”Nipende kutumia nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kenya kwa kuendesha chaguzi za wazi, huru na utulivu , aidha kumpongeza tena Rais Ruto kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya na nikutakie kila lakheri katika majukumu yako ya kuongoza nchi ya Kenya,”amesema Rais Samia.

Kuhusu ziara ya Rais Ruto nchini Tanzania, Rais Samia amesema ni fursa nyingine adhimu na muhimu sana kwao kama viongozi wakuu wa nchi zote mbili kwani inawawezesha kukaa pamoja kama majirani na ndugu wa damu kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa maendeleo na ustawi wa mataifa yao.“Pia ni fursa inayotuwezesha kutathimini masuala mbalimbali ya uhusino wetu katika ngazi zote.”


Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto akizungumza mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (pichani kulia),Wageni waalikwa pamoja na Vyombo vya habari, leo Oktoba 10,2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.
 
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya akitazama mfumo wa gari unaotumia gesi asili mara baada ya kutembelea Taasisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT) Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya akioneshwa baadhi ya vifaa vinavyotumika katika kutengeneza mfumo wa gari kutumia gesi asilia mara baada ya kutembelea Taasisi ya teknolojia Dar es Salaam (DIT)   Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya akizungumza na watumishi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) mara baada ya kutembelea Taasisi hiyo Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba akizungumza na kumkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya mara baada ya kutembelea Taasisi hiyo  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya (katikati) akiwa pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba.

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Prof Mark Mwandosya amezitaka Taasisi za Teknolojia nchini zimetakiwa kuendeleza na kuibua bunifu mbalimbali ambazo zitaweza kuimarisha amendelea ya miundombinu ya kiuchumi nchini.

Akizungumza mara baada ya kutembelea DIT leo Oktoba 3,2022 Jijini Dar es Salaam Prof. Mwandosya amesema nchi kama India na nchi nyingine zilizoendelea zimekuwa zikitumia sayansi na teknolojia katika kuwainua vijana na kupambana na umasikini na kupelekea kukua kiuchumi kwa kiasi kikubwa.

Amesema taifa likiwekeza kwenye Taasisi za teknolojia nchini tunaweza kufiika mbali na kuweza kushindana na wenzetu ambao mpaka sasa wameendelea kutokana na kuwekeza kwa muda mrefu kwenye sayansi na teknolojia.

Amesema uhusiano kati ya EWURA na DIT usiishie kwenye gesi bali waendelee kushirikiana kwenye masuala mbalimbali ambayo yatasaidia kulipelekea taifa mbele kiuchumi.

Pamoja na hayo Prof.Mwandosya ameipongeza DIT kwa kuhakikisha wanafanikiwa kubuni na kutengeneza mfumo wa magari kutumia gesi asilia.

Na Mwandishi wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amehimiza kuwa na vikao vya uratibu vya pamoja kati ya wizara na taasisi zinazotekeleza mradi wa mradi wa AFDP ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe.  George Simbachawene alipotembelea shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) Kigamboni Jijini Dar es salaam ambalo linatekeleza programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi katika mradi wa AFDP unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu sera Bunge na Uratibu na kutekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi – Zanzibar.

Waziri Smbachawene amesema programu AFDP ni ya miaka sita kuanzia 2021/2022 hadi 2027/2028 ambayo itagharimu jumla ya Dola za Kimarekani 77.4 millioni (Mkopo toka IFAD USD 58.8 millioni; Serikali USD 7.7 millioni; Sekta Binafsi 8.4 millioni na Wananchi USD 2.4 millioni).

 “Mradi huu wa   uchumi wa bluu ukisimamiwa vizuri utaibua shirikia la TAFICO, na utaibua uchumi wa biashara ya uvuvi zinazofanywa na sekta binafsi. “

Lazima tutengeneze kikosi kazi kitakachokuwa kinaashughulikia changamoto zinazojitokeza kutoka taasisi moja kwenda nyingine pamoja na wizara moja kwenda nyingine katika utekelezaji wa mradi, alisema Waziri.

“Eneo hili linaloshughulikiwa na shirika la TAFICO linaenda kujibu ahadi za ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.”

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema mradi huu ni mradi mkubwa sana na ni mradi wa kimkakati.

“Tuone namna ambavyo tutautekeleza huu mradi kikamilifu, spidi na kazi ya utekelezaji wa mradi bado hairidhishi.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya shirika la TAFICO Profesa Yunus Mgaya amesema wanalichukulia shirika la TAFICO kama shirika la kimkakati hasa katika dhana ya kutekeleza uchumi wa blue.

“Shirika linajukumu la kuwasaidia wavuvii wadogo wadogo hasa katika kunyanyua  vipato vyao, kuwawezesha kuhifadhi mazao yao ya uvuvi kuingia ubia na wananchi mbalimbali katika shughuli za uvuvi bahari kuu”

 

 

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha AICC kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulionza tarehe 21 Julai, 2022 Jijini Arusha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki kwenye Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulionza tarehe 21 Julai, 2022 Jijini Arusha
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais wa Burundi Mhe. Évariste Ndayishimiye mara baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha AICC kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulionza tarehe 21 Julai, 2022 Jijini Arusha.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ulionza tarehe 21 Julai, 2022 Jijini Arusha



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na baadhi ya Viongozi Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Wawakilishi wakati wa Wimbo wa Taifa wa Afrika Mashariki ukipigwa kwenye ukumbi wa Mikutano wa AICC Jijini Arusha kabla ya kuanza kwa Kikao cha Wakuu hao wa Nchi tarehe 21 Julai, 2022.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais wa Somalia Mhe. Hassan Sheikh Mohamud kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC Jijini Arusha tarehe 21 Julai 2022.

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiagana na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati akielekea nchini Uganda kwa Ziara ya Kiserikali ya siku mbili. Tarehe 10 Mei 2022.

 


Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza mkakati wa kubana matumizi ya Serikali katika bajeti ya matumizi ili kupata fedha za kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta linalosababisha kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma nchini.

Rais Samia ameyasema hayo jana Jumatatu Mei 9, 2022 katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari akisema Serikali imesikia kilio cha wananchi cha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

“Katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu tutachukua hatua mbalimbali za kikodi kuweka ahueni kwa wananchi.

“Hata hivyo, kutoa nafuu za kupanda kwa bei za mafuta hakuwezi kusubiri hadi mwaka huu wa fedha, nimeamua kwa hiyo wananchi waanze kupata nafuu kuanzia tarehe Mosi Juni.

Nimeelekeza kwamba, Serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka kwenye matumizi ya kawaida ya Serikali ili ziende kutoa nafuu za bei ya mafuta kuelekea mwaka wa fedha,” amesema Rais Samia.

Amemwagiza Waziri wa Nishati kutoa ufafanuzi kesho Bungeni kuhusu hatua hiyo, huku akimwelekeza Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kutoa ufafanuzi wa kodi katika mafuta.

Amesema ongezeko la bei ya mafuta limetikisa nchi zote duniani, tajiri na masikini, zenye kuzalisha mafuta na zenye kuagiza na kwamba Tanzania haijasalimika.

“Novemba mwaka jana nilielekeza tupunguze tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali. Hatua hiyo ilisababisha Serikali kupungukiwa kwa mapato yake kwa kiasi ccha Sh102 bilioni.

Pamoja na hatua hizo bado nafuu haikupatikana kutokana na kasi ya kupanda bei,” amesema.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo amemuwakilisha Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Kenya ,Hayati Emilio Mwai Kibaki. Ibada ya kumuaga Hayati Mwai Kibaki imefanyika katika Uwanja wa Nyayo uliopo Nairobi nchini Kenya na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta.





Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, wawakilishi wa taasisi za kitaifa na kimataifa pamoja na mabalozi, wananchi wa Kenya na nchi jirani wamehudhuria kuagwa kwa Hayati Mwai Kibaki.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu akiwa katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change), Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.