Mahakama katika mji mkuu wa Uganda Kampala imemhukumu kifungo cha maisha jela mfanyabiashara wa pembe za ndovu. Pascal Ochiba alikamatwa Januari mwaka huu akiwa na vipande viwili vya pembe za ndovu vyenye uzani wa karibu kilo 10. Hakimu alisema kuwa Bw Ochiba alikuwa amerudia kosa kwa mara nyingine na anastahili adhabu ya juu zaidi, kwa ulinzi wa siku zijazo wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka. Mnamo Julai 2017, Bw Ochiba alikamatwa akiwa na vipande vinne vya pembe za ndovu na ngozi ya okapi na kupelekwa gerezani. Okapi ni wanyama adimu wa msituni wenye alama kama pundamilia na wanapatikana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, Sam Mwandha, alielezea uamuzi huo kama mafanikio ya kihistoria katika vita dhidi ya biashara haramu ya wanyamapori. Mnamo mwaka wa 2019, nchi ilipitisha sheria ya kifungo cha maisha kwa watu wanaopatikana na hatia ya ujangili au usafirishaji wa wanyama walio hatarini kutoweka. Kuna tembo zaidi ya 7,900 waliobaki porini nchini Uganda, na wanyama hao wako hatarini kutoweka. #CHANZO:BBC
Share To:

Post A Comment: