Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amevitaka vikundi vya Ulinzi na Usalama vinavyoshiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kwa majeshi ya nchi za Afrika ya Mashariki kuhakikisha vinaliwakilisha vema taifa la Tanzania ili kujenga ushirikiano mzuri na nchi jirani.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa zoezi hilo linalofanyika katika mji wa Musanze, Rwanda, Jenerali Mkunda alisema kuwa zoezi hilo liwe chachu ya kujifunza namna ya kutatua changamoto za kiulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa wananchi wanayategemea zaidi majeshi yao kuwapatia msaada wa ulinzi na uokozi pindi majanga yanapotokea.

“Unajua hakuna kitu kikubwa ambacho huwa kinarudisha na kujenga imani ya wananchi kwa majeshi yao kama kupewa msaada wa kijamii pindi wapatapo majanga. Imani yao kubwa hubaki kwa wanajeshi ambao ndio huwa wa kwanza kutoa msaada.” Alisema Jenerali Mkunda.

Jenerali Mkunda pia amevitaka vikundi vinavyoshiriki kwenye zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kudumisha udugu na ushirikiano wa majeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

“Nchi yetu ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikisifika kwa kuwa marafiki wa kweli katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na dunia nzima, hivyo hakikisheni mnaendelea kuwa mfano wa kuigwa”, alisisitiza Jenerali Mkunda.

Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa zoezi hilo kwa taasisi na mamlaka za kiraia, Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Gerson Msigwa alisema kuwa huu ni wakati muafaka wa kufanya kazi pamoja kwani pindi majanga yanapotokea, mamlaka mbalimbali zinahusika kutoa utaalam wa kukabiliana na majanga hayo.

“Tupo tayari kufanyakazi na Majeshi ya Ulinzi na Usalama kuhakikisha  kuwa tunatekeleza majukumu yetu ya kihabari kusaidia kufanikisha majukumu ya kulinda amani na kurudisha imani ya wananchi pale majanga yanapotokea”, alisema Bw Msigwa.

Zoezi hilo la wiki mbili limefunguliwa rasmi Jumapili na Waziri wa  Ulinzi wa Rwanda Mhe. Juvenal Marizamunda    ambaye alimkabidhi Bendera ya kuashiria kuanza kwa zoezi Mkuu wa Zoezi hilo Dk. Alice Urusaro Uwagaga Karekezi ambaye naye alikabidhi bendera hiyo kwa Mkuu wa Majeshi ya Kikanda ( REMIKA)  Brigedia Jenerali Julius Gambosi.

Zoezi linalenga kuvijengea vikundi vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za kiraia uwezo wa kukabiliana na  Ugaidi,Uharamia, Menejimenti ya Majanga pamoja na Ulinzi wa Amani katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Washiriki wa zoezi hilo ni pamoja na Majeshi ya Ulinzi, Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Kituo cha Taifa cha kukabiliana na Mapambano dhidi ya Ugaidi. Aidha, Taasisi za Kiraia zilizoshirikishwa ni pamoja  na zilizo chini ya  sekta za Habari, Haki za Binaadam, Usawa wa Kijinsia pamoja na Diplomasia na Ushirikiano wa Kimataifa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Share To:

Post A Comment: