MAGAVANA wa Benki Kuu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoendelea kujitokeza duniani, huku migogoro ya kimataifa na mfumuko wa bei vikitajwa kuwa miongoni mwa vihatarishi vikubwa vya ukuaji wa uchumi wa ukanda huo.
Akizungumza katika mkutano huo leo Juni 11, 2026 Jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amesema ukanda wa SADC unakabiliwa na mazingira magumu ya kiuchumi yanayochochewa na migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati, hali inayohitaji nchi wanachama kuratibu kwa karibu sera zao za fedha na uchumi.
“Tumekutana katika kipindi ambacho ukanda wetu unakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi zinazosababishwa na migogoro inayoendelea Mashariki ya Kati. Mkutano huu unatupatia fursa ya kutafakari kwa pamoja changamoto hizi na kuratibu mikakati ya kukabiliana nazo nchini Tanzania na katika ukanda wetu kwa ujumla,” amesema Bw. Tutuba.
Mkutano huo uliwakutanisha magavana wa benki kuu na maafisa wakuu wa sera za fedha kutoka nchi 16 wanachama wa SADC kwa lengo la kupitia mwenendo wa uchumi wa ukanda na kujadili hatua za kukabiliana na hatari mpya zinazoweza kuathiri maendeleo ya kiuchumi.
Majadiliano yamejikita katika kudumisha uthabiti wa bei, kuboresha mifumo ya malipo, kuimarisha ukwasi wa sekta ya benki na kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wananchi na sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Aidha, nchi wanachama zimeendelea kutekeleza hatua za pamoja za kikanda pamoja na sera mahsusi za kitaifa zinazolenga kupunguza athari za changamoto za kiuchumi na kulinda ustahimilivu wa mifumo ya kifedha.
Bw. Tutuba alisema benki kuu za SADC zitaendelea kushirikiana katika kuboresha mifumo ya malipo, kuimarisha huduma za kifedha na kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa sekta ya fedha na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi katika ukanda huo.
Licha ya changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara. Sekta ya fedha imeendelea kuwa thabiti na salama, hali inayosaidia kupunguza athari za mishtuko ya kiuchumi kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa katika mkutano huo, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2 mwaka jana na unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka huu kutokana na uwekezaji unaoendelea pamoja na misingi imara ya uchumi wa taifa.
Hata hivyo, viongozi hao walibainisha kuwa pamoja na mfumuko wa bei kubaki ndani ya kiwango kinacholengwa na Benki Kuu, bado kuna umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaenda sambamba na uthabiti wa bei.
Kwa upande wa ukanda wa SADC, mkutano huo unatarajiwa kuibua mikakati ya pamoja ya kudhibiti mfumuko wa bei, kuimarisha mifumo ya malipo, kupanua huduma za kifedha na kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu huku ukihakikisha uthabiti wa sekta ya fedha unaendelea kulindwa.
Washiriki pia wanajadili namna ya kuharakisha matumizi ya teknolojia za malipo kidijitali na kuimarisha ushirikiano katika huduma za kifedha ili kusaidia ujumuishaji wa uchumi na biashara ndani ya ukanda wa SADC.
Mkutano huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania, hatua inayotambua mchango wake katika usimamizi wa sera za fedha, maendeleo ya sekta ya fedha na mageuzi ya mifumo ya malipo yaliyosaidia kuongeza ujumuishaji wa kifedha na ufanisi wa miamala nchini.

Post A Comment: