Na Ashura Mohamed, ARUSHA

Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha IAA, Dkt. Grace Temba, amezindua na kuweka msingi wa maandalizi ya kongamano la kimataifa la utalii linalotarajiwa kufanyika tarehe 25 Septemba, 2026 mkoani Arusha.

Tukio hilo la kongamano ni muhimu kwa taasisi hiyo na maalum kwa wadau wa utalii kutoka maeneo mbali mbali duniani likilenga wadau wa sekta ya utalii kwa dhima kubwa ya kuhamasisha utalii wa ndani ili kuendelea kuhamasisha idadi ya watalii kuongezeka.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Dkt. Grace amesema kuwa lengo hasa ni kuhakikisha wadau mbali mbali wanashiriki na kufanya kongamano hilo kujumlisha watunga sera, wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya nchi kujiandaa na kushiriki kwa ufanisi zaidi.

“Siku ya kongamano tunawaweka pamoja wadau mbali mbali tunatoa taarifa mbali mbali za utafiti zilizofanywa na wadau mbali mbali waliopo katika sekta ya utalii lakini pia Chuo cha Uhasibu Arusha, watunga sera wa taasisi na mlaji ili kuja na suluhisho na maboresho makubwa katika sekta ya utalii kwa lengo la kunufaisha pande zote,” alisema Dkt. Grace.

Aidha amesema kuwa kongamano hilo la nne linatarajiwa kuendelea kukuza na kutangaza nchi kimataifa kwa kuja na mawasilisho ambayo yatalenga wadau na watoa huduma kuendelea kujikuza kimasoko, miundombinu, na kuifanya sekta hiyo kuwa bobezi na kuchangia pato la taifa.

Nae Kaimu Mkuu wa Kitivo cha Biashara na Sayansi ya Jamii kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha IAA, Bi. Lorna Boniface Mwijarubi, amesema kuwa chuo hicho kinatarajia kushirikiana na taasisi mbali mbali na wadau wa utalii katika kuonyesha tafiti na bunifu ambazo zitaisaidia sekta ya utalii kuwa bora zaidi na kuendelea kuliingizia taifa kipato.

Amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na makongamano yaliyopita ni makubwa kwa kuwa yamekijengea chuo mashirikiano na wadau ambayo huwezesha wanafunzi wa kozi ya utalii na ukarimu kupata fursa ya kujifunza kwa vitendo katika maeneo mbali mbali nchini na kusaidia kupata ajira pamoja na taifa kupata mapato kupitia sekta hiyo.

Chuo cha Uhasibu Arusha IAA kimeendelea kuwa maarufu katika sekta mbali mbali kwa kutoa elimu bora yenye ushindani sokoni huku katika sekta ya utalii inatajwa kuwa ndio chuo pekee kinachotoa kozi ya utalii na ukarimu nchini ambayo inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kutangaza nchi na kuendelea kuifanya sekta hiyo kuwa bora zaidi nchini.











Share To:

Post A Comment: